Week Hot newz

Papa kuongoza Karamu ya Mwisho ya Bwana katika kituo cha Walemavu


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamis Kuu majira ya jioni, saa 11:30, ataadhimisha Karamu ya Mwisho ya Bwana, na liturujia ya kuosha miguu watu kadhaa kama ishara ya unyenyekevu na huduma, akiwa katika Kituo walemavu cha Shirika la Mtakatifu Maria wa Kudra ya Mungu, cha Shirika la la Don Gnocchi, cha mjini Roma. Shirika hili hufadhili watu wapatao elfu tatu wenye ulemavu na tegemezi nchini kote Italia, Rome kukiwa na vituo vyake 12 ambavyo hufadhili wageni wahitaji wanaoingia jiji la Roma, kati ya vituo vya 29 vinavyofanya kazi katika mikoa tisa ya Italia.

Baba Mtakatifu Francisko anasubiriwa kwa hamu na wagonjwa na familia zao katika cha kituo cha Mtakatifu Maria wa Kudra ya Mungu , mtaa wa Via Casal Marmo 401, Roma , ambako watu wa kujitolea huhudumia wagonjwa na familia zao. Alhamis Kuu ya mwaka jana Papa Francisko aliadhimisha pia Ibada ya Alhamis Kuu akiwa katika gereza la watoto la mjini Roma.
Kwa Alhamis Kuu hii, taarifa zinaeleza kwamba, tukio hili la Baba Mtakatifu, kukitembelea Kituo cha Waelmavu cha Don Gnocchi, linafanyika baada ya kupita wiki chache kwa shirika hili kuadhimisha sherehe kubwa ya kupita kwa miaka mitano tangu mwanzilishi wa shirika Don Gnocchi kutajwa Mwenye Heri Februari , sherehe iliyohudhuriwa na waelfu ya waamini, kama sehemu ya mipango kwa ajili ya maadhimisho ya miaka tano ya Don Carlo Gnocchi , kutajwa Mwenye Heri. Sherehe zilizo hamasisha mwamko mpya wa utamaduni wake wa muda mrefu na huduma maalum, isiyoweza kusahaulika, inayoonyesha kupandwa kwa Mbegu ya mshikamano na umoja kwa jirani katika utendaji wa Papa, " baba wa vilema ".

Kituo cha Mtakatifu Maria wa Kudra ya Mungu , ambacho zamani kilifanya kazi kwa jina la Mama Nasi, nyumba ndogo ya Maongozi ya Mungu ya Cottolengo, ilifanywa kuwa Shirika la Don Gnocchi Foundation Septemba 2003 na kwa sasa lina jumla ya 150 vitanda, ambamo kuna makazi kwa ajili ya huduma ya Afya kwa Watu wenye ulemavu 60 vitanda, ambao hawahitaji kuunganisha na vifaa vya aina hospitali au vituo vya ukarabati ); na pia kuna idara ya kisasa ya ukarabati wa mwili “ neuromotor” wa ngazi ya juu, wanaotumia vitanda 60 , ambao pia hupokea huduma ya mazoezi ya mwili, , huduma ya tiba , tathmini saidizi teknolojia na ushauri nasaha, nasaha za kisaikolojia na elimu kwa shughuli zinazo husiana na hali ya wagonjwa hao. Na vitanda 30 vilivyo baki , ni kwa ajili ya wanaotoa huduma kwa wagonjwa.

Mbali na huduma hiyo ya ndani pia huhudumia wagonjwa walemavu kama wagonjwa wa nje kila siku, ambao hupewa tiba na ushauri wa ukarabati na huduma za nyumbani .

Rais wa Shirika la Don Gnocchi, Mosinyori Angelo Bazzari , akizungumzia Papa Francisiko kuendesha Ibada ya Karamu ya Bwana katika kituo hicho cha Mtaa wa Via Casal Marmo , amesema ni furaha kubwa kwao na wanamkaribisha Baba Mtakatifu kwa furaha kubwa ndani mwao. Na kwamba, ishara ya kuosha miguu ni wazi inayoonyesha kwamba Kanisa tangu kuanzishwa kwake, daima limeitwa kuhudumia kwa unyenyekevu hasa watu masikini na dhaifu. Ni huduma ya upendo wa Papa katika ulimwengu wa mateso na ishara ya huruma ya Kiiinjili, ambayo husaidia kukumbuka kwamba , kiwango cha ustaarabu wa jamii kinapaswa kuwa kipimo katika uwezo wake wa kutembea pamoja na watu dhaifu.

Upendo huu wa kuhudumia dhaifu na wanyonge katika jamii, ni karama ya Don Gnocchi , aliyowaachia kama urithi wafanyakazi zaidi ya elfu tano wa Shirika lake, ambayo hufanya kazi kila siku kwa majitoleo ya bila kujibakiza , kwa uaminifu na kama msimamo kila siku , katika dhamira yao ya uwezo, nia, huduma na uendelezaji wa maisha ya maelfu ya watu wanaotafuta huduma katika vituo vya shirik, kwa ajili ya Utafiti wa Afya , mshikamano na huduma.

Papa atoa zawadi ya Injili kwa wafungwa

Papa Francisko atatoa vItabu vya Injili vidogo vinavyoweza kuwekwa mfukoni, vipatavyo elfu moja mia mbili, kama zawadi ya Pasaka kwa wafungwa katika Gereza Kuu la Malkia wa Mbingu la Roma. Zawadi ya Papa itawasilishwa Jumatano hii, na Askofu Mkuu Konrad Krajewski wakati atakapo tembelea jengo la Gereza katika mtaa wa Lugara Roma.
Kitabu hicho kidogo cha Injili chenye kuwa pia waraka wa Matendo ya Mitume, Jumapili iliyopita pia kiligawiwa kwa waamini waliofika kumsikiliza Papa wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana katika uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, na pia kwa waliohudhuria Ibada ya Misa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu George Mkuu la Magliana Roma.

Na Jumapili ya tarehe 4 Mei, Papa ana mpango wa kufanya ziara ya Kichungaji katika Kanisa la Mtakatifu Stanslao la Botteghe la Roma.
Kisha 18 Mei 2014 , majira ya saa kumi za jioni , Papa Francesko atafanya hija katika Madhabahu ya Bikira Maria wa Upendo wa Mungu, ambayo yako katika Mtaa wa Via Ardeatina nell’Angola Romano , nje kidogo ya jiji la Roma. Hija inayopendwa na watu wa Roma.
Madhabau ya Bikira Maria wa upendo wa Mungu, ya Mtaa wa Via Ardeatina , yako kiasi cha umbali wa kilomita 12 Roma, katika kanda ya Agro Romano katika jengo la Castel di Leva. ambalo kwa mara ya kwanza liliteuliwa na Papa Gregoria V11 kwa barua yake ya kitume ya mwaka 1081, kama mali ya Abassia ya Mtume Paulo . Na mwaka 1268, mali hiyo ililithishwa kwa Kanisa la Mtakatifu Sabina na baadaye kupewa Wana shirika wa Orsinina mwaka 1295na tena kuhamishiwa kwa Wasaveli.
Na baada ya kupitia katiak mbadiliko mbalimbali, Desemba 1938, Madhabahu hayo yalifanywa kuwa Parokia ikiongozwa na Paroko wa kwanza Don Umberto Terenzi ambaye mwaka 1942 alianzisha Shirika la Mabinti wa Maria wa Upendo wa Mungu na mwaka 1962, madhabahu hayo yakawekwa chini ya usimamizi wa Shirika la Oblates hadi leo. Simulizi juu ya madhabahu hayo, huelezea tukio la mwaka 1740, juu ya muujiza uliotokea kwa muhujaji mmoja aliyekuwa akisafiri kwenda Roma kuhiji ambaye alipofika katika eneo hilo, kulitokea kundi la mbwa mwitu wakali walotaka kushambulia, lakini mara aliomba msaada wa Mama Bikira Maria na ghafla mbwa wao walizuiwa na kitu kisichoonekana na kutoweka zao. Aidha watu wa Roma wanasadiki, Sanamu ya Bikira Maria wa Upendo wa Mungu iliyo katika eneo hili iliweza kuuokoa mji wa Roma dhidi ya kuanguka katika mikono ya maadui wakati wa vita kuu ya pili ya dunia.

Ushuhuda wa kuokelewa na Bikira Maria wa Upendo wa Mungu, ndiyo asili ya hija katika eneo hili ambako waamini wanapenda kwenda kuomba msaada wa kwa Bikira Maria kutatua shida zao mbalimbali na pia kwa ajili ya kutoa shukurani zao kwa mambo mbalimbali waliyofanikisha.



Maadhimisho ya Juma kuu ili kuadhimisha Fumbo la Pasaka




Maadhimisho ya Jumapili ya Matawi, Kanisa linamshangilia Kristo alipoingia Yerusalemu kwa shangwe na watoto wa Wayahudi wakatandaza nguo zao njiani. Hii ni siku ya vijana kijimbo, inayoongozwa na kauli mbiu, "Heri maskini wa roho maana ufalme wa mbingu ni wao".

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kubariki matawi, umati wa vijana ulianza maandamano kuelekea kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, huku wakiimba kwa shangwe. Baba Mtakatifu katika Ibada hii ametumia Fimbo ya Kiaskofu aliyozawadiwa na wafungwa kutoka gereza la Sanremo, Italia. Huu ni mwanzo wa maadhimisho ya juma kuu, Kanisa linapokumbuka mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake anatawaka waamini kujitafakari kwa kuangalia hali yao mbele ya Yesu, kama wako kweli na hamasa ya kuonesha furaha na kumshangilia, au wamejikunyata na kumwangalia tu kama "nyanya mbichi". Katika shida na mahangaiko ya Yesu, waamini wanajisikia namna gani na wako upande gani? Je, ni kati ya kundi la wakuu wa Makuhani na Waandishi waliokuwa wanasubiri fursa ya kumkamata na kumsulubisha Yesu?

Je, wao pia ni sehemu ya akina Yuda Iskarioti waliomuuza Yesu kwa vipande thelathini vya fedha? Au ni kati ya Mitume waliokuwa wanauchapa usingizi wakati Yesu anakabiliana na mateso makali? Baba Mtakatifu anawauliza waamini ikiwa kama wanataka njia ya mkato kwa kutumia upanga kama ambavyo alitaka kufanya Mtakatifu Petro? au Yuda aliyemsaliti Yesu kwa busu la unafiki? Au Wazee wa Baraza wanaofanya kila mbinu kwa kutafuta mashahidi wa uwongo ili kumtia Yesu hatiani kwa kudhani kwamba ni kwa ajili ya mafao ya wengi?

Baba Mtakatifu anaendelea kuwauliza waamini ikiwa kama wanafanana na Pilato anapoona kwamba, "maji yamezidi unga" ana nawa mikono ili kukwepa wajibu wake kwa kuwashirikisha wengine. Katika hali ya kuchanganyikiwa na vurugu, Je, hata waamini nao wanaendelea kupiga kelele wakitaka Barabara afunguliwe na Yesu ahukumiwe kifo ili kuwafurisha watu na kumdhalilisha Yesu au kama wale Askari waliomdhihaki, wakampiga mijeledi na kumtemea mate usoni?

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake ambayo yalikuwa ni tafakari inayomshirikisha mwamini binafsi anawauliza ikiwa kama kweli wamekuwa na ujasiri wa Simoni wa Kirene aliyeshurutishwa kumsaidia Yesu kubeba Msalaba wake naye kwa upendo mkubwa akatekeleza dhamana hii! Kuna watu waliokuwa wanapita mbele ya Msalaba wakimdhihaki Yesu kwa vile alijiaminisha kuwa ni Mwana wa Mungu. Baba Mtakatifu anawauliza waamini, Je, hata wao wanajisikia kuwa na jeuri hata kumdhihaki na kumkejeri Mwana wa Mungu?

Bikira Maria na baadhi ya wanawake wajasiri, walisimama chini ya Msalaba kwa ujasiri mkubwa, wakateseka pamoja na Yesu katika hali ya ukimya!, Je, waamini nao wanaendelea kuteseka na Yesu katika hija ya maisha yao ya kila siku, tayari kama Yusufu wa Arimatayo kwenda kuchukua Mwili wa Yesu ili kuuzika au wanawake waliokuwa wanalia mbele ya kaburi la Yesu au wale Askari walioomba ulinzi mkali kwenye Kaburi la Yesu aliyekuwa ametangaza kwamba, baada ya Siku tatu angefufuka kutoka katika wafu? Hawa ni watu waliokuwa wanataka kuzuia maisha mapya kwa njia ya ufufuko wa Yesu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, haya ni maswali msingi ambayo yanaweza kuwasaidia waamini katika tafakari ya maadhimisho ya Juma kuu, Kanisa linapotafakari Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo.

Amepanda Punda na wala si Prado, lakini Yesu anafunika! Wamemkubali!



Katika ulimwengu wa leo suala la maandamano limeshamiri karibu katika kila nchi. Maandamano hayo yanakuwa ya jamii fulani inayodai haki yake, mathalani yanaweza kuwa maandamano ya wanawake wanaodai haki zao za kijinsia, wafanyakazi, wanafunzi, waganga nk.

Maandamano mengine yanakuwa ya kufanya kampeni ya uongozi, na mengine ni ya shamrashamra za sikukuu fulani za kidini au arusi nk. Maandamano yoyote yanakuwa na sehemu mbili maalumu yaani pahala pa kuanzia na pa kumalizikia, sehemu hizo zaweza kuwa hospitalini, shuleni, uwanjani, ikulu au hata kanisani nk.

Leo tutayaona maandamano ya namna yake yanayoendeshwa na Yesu. Maandamano hayo siyo ya kufanya mgomo wa madai ya masilahi toka serikalini, la hasha, bali tungeweza kuuingiza kwenye aina kama vile ya kampeni ya kupigania sera zake za uongozi. Maandamano hayo yalikusanya watu wengi sana, wakiwepo wanafunzi wake, mashabiki wengi na wapambe kibao mpaka mji ukatikisika. Yerusalemu hapakutosha! Mapato yake hata viongozi wa dini na wa serikali walipoyaona maandamano hayo wakataharuki na kuulizana: “Ni nani huyu?”

Maandamano ya leo yalianza pahala palipoitwa Bethfage na yakaishia mjini Yerusalemu tena ndani ya Hekaluni. Humo hekaluni, Yesu anahitimisha maandamano siyo kwa kutoa hotuba refu ya ahadi hewa, hapana, bali kwa kuwashughulikia watu waliokuwa wanachenji hela na kufanya biashara ndogondogo hekaluni, halafu siku ya pili yake anapokuwa na njaa anaulaani mtini usiozaa matunda.

Sasa hebu tupaone kwanza pahala palipoanzia na palipoishia maandamano hayo, yaani Bethfage na Yerusalemu. “Hata walipokaribia Yerusalemu, na kufika Bethfage, katika mlima wa Mizeituni.” Bethfage, ipo upande wa Mashariki ya mlima wa Mizeituni, baada tu ya Bethfage kuna mlima wa Mizeituni ambako ukisimama juu yake unaweza kuangalia vizuri sana mji wa Yerusalemu ulio chini yake. Neno hili Bethfage ni muunganiko wa maneno mawili, Beth (Bayet) ni nyumba; na Fage ni matunda ya tini yasiyokomaa. Kwa hiyo Bethfage ni nyumba ya matunda ya tini yasiyokomaa.

Jambo la kushangaza ni kwamba baada ya kuingia Yerusalemu na kuwasambaratisha wafanyabiashara hekaluni, linafuata simulizi la mfano ule ambao unonesha kitu gani Mungu anakitegemea toka kwa Taifa lake, yaani kitendo cha Yesu kwenda kutafuta matunda kwenye mti wa mtini na bila kukuta kitu isipokuwa majani matupu, anaulaani. “Mtini ukanyauka mara.” Tendo lile la Yesu ni mfano hai unaolingana na kile anachokitegemea Mungu toka kwa watu wake kifanyike ndani ya hekalu au katika ibada zao, lakini anakikosa.

Mungu anategemea kupata matunda ya upendo, ya haki, ya kuwajali maskini, wajane, yatima na watoto, wageni, badala yake ndani ya hekalu anakuta majani, yaani, liturjia, nyimbo za kupendeza, madhehebu marefu, chetezo, ubani na mishumaa kwa wingi. Vitu hivi havisemi chochote kile mbele ya Mungu kama havizai matunda. Hivyo siyo sadaka ambazo Mungu anategemea kuziona toka kwa watu, kwake Mungu vitu hivyo ni kama majani tu, au ni kama Bethfage tu (matunda yasiyokomaa).

Baada ya kuona maana ya mandhali ya maandamano, sasa tuwaone wahusika wakuu wa maandamano hayo. Anapofika Bethfage anawaagiza wanafunzi wake wamletee usafiri: “Enendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, na mara mtaona punda amefungwa, na mwanapunda pamoja naye. Wafungueni mniletee. Na kama mtu akiwaambia neno, semeni, ‘Bwana ana haja nao,’” Maagizo haya ni ya muhimu sana na umuhimu wake unaonekana jinsi masimulizi yanavyorudi mara mbili. Mosi, pale anapowaagiza mitume wake: “mtaona Punda amefungwa, na mwanapunda pamoja naye. Wafungueni mniletee.” halafu inarudiwa tena inaposemwa. “Wale wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaamuru (kuwafungua), wakamleta yule punda na mwanapunda”. Msisitizo upo katika kuwafungua hao punda na kuwaleta ili waweze kutumika kwa kazi atakayoitaka Yesu waifanye. Endapo maandamano haya ni ya kampeni za uongozi, basi yaonekana siri na sera za uongozi huo zimelala katika Punda hao. Kwa hiyo Punda ndiyo wasanii wakuu wa maandamano ya leo.

Kazi ya wanafunzi waliotumwa ni kuwafungua punda. Wanyama hawa punda wana maana gani katika Biblia? Mfalme wa enzi za Wayahudi aliwastaajabia sana Farasi na wapanda Farasi waliojulikana kuwa hodari kwa kupigana vita. Kwa mfano, tunasikia kuwa askari wa Farao Farasi na wapanda Farasi wao wote waliangamizwa baharini. Hivi hata Wafalme wa kiyahudi walikuwa wanatamani sana kuwa na farasi na wapanda farasi. Katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati, mfalme Salomoni anaonywa asiongeze idadi ya Farasi, na asiuze ndugu zake kwa Wamisri kwa ajili ya kuwa na Farasi na wapanda Farasi (askari). Kutembea juu ya farasi ni alama ya ukuu, uongozi, utawala, ufalme, utajiri na ufahari. Namna ya usafiri unaonesha hadhi ya mtu.

Siku za leo, tunaweza kupata picha ya magari ya gharama na ya fahari wanayotembelea marais, mawaziri, wabunge, makardinali, maaskofu, matajiri, maofisa, nk Itakuwa ni kichekesho na haiwezekani kabisa kumwona kiongozi wa hadhi kama hizo kusafiri kwa lori la mkaa, kwa Bajaji au kwa bodaboda, au baiskeli nk. Katika kampeni za uongozi wa kisiasa, wagombea wanasafiri kwa magari ya gharama za kutisha, kama vile gari aina ya Prado, VX, Helikopta. Hii ndiyo hadhi yao.

Kumbe, katika maandamano ya kampeni za Yesu, anamchagua Punda jike na mwanapunda kuwa prado ya kuingia nayo rasmi mjini Yerusalemu. Hii ndiyo sera mpya ya utawala na uongozi anaotaka Yesu kuuingiza ulimwenguni. Ni kiongozi pekee anayefanya hivyo. Marko anasema kwamba hakukuwahi kutokea mtu mwingine yeyote yule aliyewahi kumpanda yule Punda kabla: “Mtamwona mwanapunda amefungwa, asiyepandwa na mtu bado” (Mk. 11:2). Tamko hilo la Marko ni muhimu sana, likimaanisha kwamba, hakujawahi tokea mfalme au rais yeyote yule hapa duniani, aliyewahi kujionesha, katika hali kama hii ya utumishi. Yesu ni mfalme wa kwanza na wa mwisho anayependekeza aina hii mpya ya utawala.

Ili kuelewa vizuri ujumbe tunaoletewa hapa hatuna budi kuangalia mwishoni mwa kitabu cha Mwanzo ambako Yakobo anatoa baraka yake kwa watoto wake kumi na wawili, anapotoa baraka kwa Yuda, ambaye ni mtoto wake wa kwanza na atakayekuwa kiongozi wa kabila la Israeli, anasema: “Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, wala mfanya sheria kati ya miguu yake, hata atakapokuja Yeye, mwenye milki, ambaye mataifa watamtii. Atafunga punda wake katika mzabibu, na mwanapunda wake katika mzabibu mzuri.” (Mwanzo 49:10-11). Sisi hapa tuko mbele ya kituko hicho cha Yesu anayemfungua punda na mwanapunda kama rejea ya Yuda, yaani yule ambaye ataingiza sera za uongozi, utawala mpya ambao hautakuwa na mwisho. Sasa amefika yule ambaye ni kiongozi mpya wa taifa.

Yesu anasema: ‘Wafungueni mniletee’ Wasanii wakuu tunaoletewa hapa leo, wanayo tabia ya pekee sana. Mnyama huyu anafugwa na kuthaminiwa na binadamu hasa kutokana na tabia yake ya kufanya kazi. Kutokana na tabia hiyo, mnyama huyu anayo majina mengine mengi sana yanayowakilisha udundaji wake wa kazi, wengine wanamwita, Nsikiri, Kihongo, Daqwai, Mbunda au Punda nk. Ukitaka kumsifia mtu anayefanya kazi sana wanasema: “Anafanya kazi kama kihongo.”

Hivi Punda ni alama ya kazi, utumishi, na uvumilivu, hachoki kamwe, daima yuko tayari kubeba mizigo. Tabia hii ya Punda ndiyo ilimvutia Yesu hadi akamchagua kuwa mfano wa kuigwa na kipeo cha utumishi ambao unawakilishwa katika nafsi ya kila mtu. Sisi tunashangaa tunapomwona Yesu anajilinganisha na Punda. Kumbe, yeye alitaka daima ajioneshe kama mtu wa kutumikia. Kwa hiyo anapoagiza “wafungueni Punda” anamaanisha kuwa, Punda hao walikuwa wamefungwa, na katika hali hiyo ya kufungwa hawawezi kufanya kazi. Ilibidi kwanza wafunguliwe ili waweze kufanya kazi.

Kila mmoja wetu anao uwezo wa kufanya kazi na uwezo wa kutumikia. Tunayo hali hiyo kutokana na kufanana kwetu na Mungu katika upendo. Upendo ni zawadi kwa maisha yetu maana yake ni kuwajali wengine, yaani kutumikia. Ndani yetu sisi tunaye huyu Punda, Kihongo, Nsikiri nk. Kwa hiyo, endapo punda hao ni sisi, basi yabidi tufunguliwe tuwe huru kufanya kazi yaani, kutumikia, kuvumilia, kunyenyekea, kuwa tayari daima... Yaani tunao uwezo wa kutumikia, lakini daima tumejifunga hatutaki kujifungua ili tuwe huru kutumikia, badala yake tunataka daima kutumikiwa.

Yesu anawapa wanafunzi wake kazi: “Enendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, mtaona Punda amefungwa, na mwanapunda pamoja naye. Wafungueni mniletee”. Kazi ya wanafunzi ni kuamsha nguvu ya kutumikia iliyo ndani yetu, kuifungua na kumpelekea Yesu.

Yesu anaongeza kusema: “na kama mtu akiwaambia neno, semeni, ‘Bwana ana haja nao’”. Maana yake akitokea mtu fulani anakataza au anaonesha kupinga. Mtu huyo si mwingine bali ni mimi ninayesema: Tafadhali uniache huru, Usimfungue punda aliye ndani mwangu. Lakini Yesu anakuhitaji anasema: “Nina haja nawe,” kwa sababu kwa njia ya ushirikiano wetu, Yesu anaweza kuanzisha utawala wake duniani kwa kishindo, lakini siyo utawala wa kukandamiza, bali wa utumishi, wa upendo, na wa haki. Yesu anahitaji mchango wa kura ya moyo wako kwa kadiri ya uwezo wako yaani ujifungue, uwe huru, ujiruhusu, kuwa na haki na upendo wa kutumikia, kuwa tayari kusaidia wengine kusudi kuunda uongozi mpya.

Nabii Zakaria anasema: “Tazama, (Yerusalemu) mfalme wako anakuja kwako, mpole, naye amepanda Punda, na mwana Punda, mtoto wa Punda.” Nabii anasema, mfalme huyo haendi vitani kama mpanda-farasi, bali amepanda punda ambaye ni kwa ajili ya kazi ya kutumikia. Kwa hiyo mfalme (kiongozi) huyo anakuja kutumikia. Wanyofu ndiyo watakorithi ulimwengu huu mpya.

Baada ya kuipata sera ya Yesu kutokana na aina ya usafiri aliotumia katika kampeni yake, sasa tuwaone waandamaji katika msafara huu wa Yesu. Punda walipowasili, “wanafunzi wakaweka nguo zao juu yao, naye akaketi juu yake. Watu wengi katika ule mkutano wakatandaza nguo zao njiani: wengine wakakata matawi ya miti, wakayatandaza njiani.” Vifaa hivi na matendo ya waandamaji ni muhimu sana katika maandamano haya. Hebu tuyafuatilie.

Tafsiri halisi ya nguo hapa ingekuwa mgolole au shuka, yaani ni nguo ya binafsi inayomsitiri mtu anapoivaa au hata kujifunika anapolala. Kadhalika kwa Myahudi, hiyo ilikuwa ni nguo yake binafsi. Ni sawa na vazi binafsi ambalo mtu huwezi ukalitoa kwa yeyote. Unaweza ukagawa kitu kingine lakini siyo shuka ya kujifunika au mgolole wa kujitanda. Kwa hiyo nguo hizo ni alama ya utu wa mtu, nafsi yake, uwepo wake na kila kitu chake.

Wanafunzi wanaweka au kutandika shuka na migolole yao juu ya Kihongo na mtoto wake, inamaanisha kwamba wao wanayatoa maisha yao na kila kitu ikiwemo utajiri wao, kwa utumishi unaopendekezwa na Yesu kutokana na tabia ya huyo Kihongo. Yesu anaikalia hiyo migololi ya wanafunzi hao kuonesha kuwa wako chini ya utawala ambao Yesu ndiye mfalme wake. Wanakubaliana na uongozi huu pamoja na sera zake. Yesu mwenyewe akiwa mnyofu, mnyenyekevu, mpole na mtii anasafiri juu ya Punda aliye mvumilivu, mfanya kazi, mtumishi tu na anakaa juu ya migololi hii ya wanafunzi. Wamepokea, na kuukubali uupya wa masiha huyu, mtumishi na mleta amani. Ndiyo maana ya kuweka migololi yao juu ya Punda.

Watu wengine wengi pia wanajitokeza kushangilia: Watu wengi katika ule mkutano wakatandaza nguo zao njiani: wengine wakakata matawi ya miti, wakayatandaza njiani.”

Watu hao wanafanya mambo tofauti na wanavyofanya wanafunzi. Wanafunzi wanatandika migololi yao juu ya punda kuonesha kwamba wao ndio wanaoendeleza sera za mtindo huo wa uongozi. Watu wengine kumbe wanatandaza nguo zao njiani au barabarani. Kiutamaduni ilikuwa kwamba, wakati wa kumtawaza kiongozi, watu walikuwa wanatandaza nguo ardhini na kushangilia ikiwa na maana kwamba walikuwa wanakubali kujitoa na kujiweka chini ya uongozi wa huyo mfalme.

Katika nafasi hiyo watu walikuwa wanashabikia na kupiga vigelegele lakini mara nyingi hawakuelewa sera za uongozi huo. Katika kundi la maandamaji wa leo yaonekana kulikuwa na wapambe wengi sana: “Watu wengi katika ule mkutano wakatandaza nguo zao njiani, na wengine wakakata matawi ya miti, wakayatandaza njiani. Na makutano waliotangulia, na wale waliofuata, wakapaza wauti wakisema, Hosana, Mwana wa Daudi; ndiye mbarakiwa, yeye ajaye kwa jina la Bwana; Hosana juu mbinguni.” Watu hawa wote walikuwa wanamshabikia mfalme huyu lakini pengine kadiri ya sera walizokuwa wanazifikiria wao.

Wanampokea lakini kadiri wanavyoelewa wao aina ya Mfalme wanayemtegemea. Ni tofauti na mitume wanaoweka nguo zao juu ya punda. Hata katika mazingira yetu ya sehemu mbalimbali yaweza kutokea wachache wanaoelewa maana ya utumishi ya kumfuata Yesu na watu wengine wakabaki ni wapambe na mashabiki tu. Watu hao wanakata na matawi ya miti kushangilia.

Kuhusu matawi ya miti, kunakumbushia Sikukuu ya Vibanda. Siku hiyo waliyakata matawi ili kusherekea kumbukumbu ya kukombolewa toka utumwani Misri. Hapa sasa wanakata matawi kuonesha kuwa sasa wanao uhuru kwa sababu Masiha amefika. Lakini Masiha huyo wanayemdhani ni wa aina gani? Hapo tunaona ukweli wa usemi kwamba “katika msafara wa mamba kenge nao hawakosekani.” Watu waliendelea kuimba “Mwana wa Daudi” lakini ni mwana wa Daudi wanayemtegemea wao.

Katika sikukuu hii ya Matawi tunaalikwa kujihoji upya ushirika wetu na Kristu. Endapo tunataka kidhati kuwa washiriki wa ufalme mpya anaotupendekezea Yesu yabidi tumfungue punda aliye ndani mwetu ili kuwa na uwezo wa kupenda ambao Mungu ametupatia. Tuwe Punda, Kihongo au Nsikiri aliyefunguliwa na kukubali kumbeba Kristu, yaani kutumikia kwa upendo.

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.

BATAROKOTA AOMBA KURA ABEBE TUZO YA KILI

Na Dina Ismail, Dar es Salaam
MSANII wa muziki wa asili nchini, Pascal linda maarufu kama Batarokota amewaomba mashabiki wa muziki nchini kumpigia kura kwa wingi ili aweze kushinda tuzo za kili mwaka 2014.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY, msanii huyo alisema kuingia kwenye kinyang'anyiro hicho kumefanikushwa na mashabiki hao hivyo amewaomba kuendelea kumpa ushirikiano kwa kumpigia kura kwa wingi.
Batarokota anaomba kura zenu

"Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sintowashukuru wadau wa muziki hivyo nawaomba waendelee kunisapoti kwa kunipigia kura",alisema
Batarakota ambaye wimbo wake wa Kwejaga Nyangisha umeteuliwa kuwania tuzo hizo kupitia kipengele cha wimbo wenye vionjo vya kitanzania amewaomba mashabiki kumpigia kura kwa kuandika ab1 kwenda no 15440.
Aidha msanii huyo mzaliwa wa Mwanza akifanya kazi zake nchini Kenya, anaimba nyimbo zake akitumia lugha za Kisukuma, Kinyamwezi na Kinyakyusa ambapo kwa sasa yupo mbioni kukamilisha albamu yake ya kwanza.
Batarokota katikati akiwa na rafiki zake Wazungu

Jumapili ya Matawi



Mpendwa mwana wa Mungu karibuni katika kipindi cha tafakari tunapoadhimisha Dominika ya Matawi, Dominika ambayo ni mwanzo wa Juma Kuu, Juma la Pasaka. Kabla ya Misa Takatifu daima tunaanza kwa maandamano ambayo ni ishara ukumbusho wa kuingia kwa Yesu Kristu Yerusalemu.

Ni ishara ya utukufu kwa Mungu juu mbinguni. Mwaliko ambao Mama Kanisa anatupa ni ule wa kumshangilia Bwana na kuandamana tukimsindikiza kuelekea Yerusalemu. Kwa kawaida yaweza kuonekana tunafanya kumbukumbu tu lakini si hivyo bali tunashika imani na tunamsindikiza na kupata neema zote alizozitoa wakati ule na tunashika njia yetu ya kumfuasa yeye tukielekea Pasaka ya Mbinguni.

Ewe msikilizaji, kwa kawaida tunajua kuwa Kristu aliteswa, akafa na kisha kufufuka, kumbe kwa njia hiyo tunapata tumaini na tunaalikwa kufuata nyayo zake daima mpaka kufa kwetu. Kwa jinsi hiyo njia ya Bwana ni njia yetu sote. Mama Kanisa ametuwekea mateso makali ya Bwana mbele yetu ambayo yaweza kuwa ni tishio na hivi kujenga woga katika safari, hata hivyo hatuogopi maana ikiwa Bwana ambaye hakustahili alivumilia, je sisi ambao twasitahili twaweza kukwepa wajibu huo? Si hilo tu bali pia matunda ya mateso makali ya Bwana tumeona ni wokovu wa ulimwengu.

Bwana anapokaribia kuingia Yerusalemu ili kumalizia njia yake ya mateso anapanda mwanapunda, hii ni ishara ya unyenyekevu, ishara ya kuwa yeye si mfalme wa mabavu bali anayetumia upendo kujibu ubaya wa ulimwengu. Hii haina maana kuwa hana uwezo, bali uwezo wake ni kwa ajili ya wokovu wa watu na si wa mapigano ya kivita.

Watu wote wanatandaza nguo na majani ya mitende wanaimba Hosana Mwana wa Daudi, hili ni shangilio kwa Mungu wa mbinguni, ni kiitikio cha utukufu na ushindi wa Bwana. Kwa hakika ni mwendelezo wa shangilio ambalo malaika walilitoa kwa Mwana wa Mungu alipozaliwa pangoni Betlehemu, (Lk 2:14). Jibu la shangilio hili tumpalo Bwana ni amani yangu nawapa, yaani amani iliyo zawadi kwetu, (Yn 14:27).

Nabii Isaya anapoagua juu ya Masiha anatuwekea Masiha aliye mvumilivu, anayetukanwa anayekubali kupigwa na hata kung’olewa ndevu lakini hajibu mapigo, bali ametulia na kuweka tumaini kwa Mungu wake. Jambo hili linakamilika katika Bwana wetu Yesu Kristo, anapoingia Yerusalemu. Mwinjili Matayo anasema tazama maaskari wa Pilato wanavyomdhihaki Yesu Mkombozi” (Mt. 27:27-31). Kwa jinsi hii Nabii Isaya anamtangaza Masiha mshindwa, mteswa, asiyeua lakini anayehuisha kwa upendo na kuleta wokovu.

Mpendwa msikilizaji, Mtume Paulo anawaonya Wafilipi na kisha kuwaimarisha katika kuiga na kujifunza kwa Bwana. Katika familia ya Wafilipi kuna chuki, ugomvi na fitina na hivi anawapa wosia akisema kila mmoja amthamini mwenzake na kwa kukazia wosia huu anaweka mbele yao Yesu Kristu Masiha aliyejishusha mpaka kuwa mwanadamu na si ubinadamu tu bali hata kuteswa na Warumi! Chukua muda kidogo tafakari na fikiri juu ya upeo wa jambo hili!

Fikirini mtu bilionea akijishusha na kukaa na maskini! Kwa hakika mbele ya ulimwengu atakuwa wa ajabu lakini wa maana zaidi mbele ya Mungu. Kristu kwa umwilisho wake hakupoteza Umungu wake bali ulibaki umejificha na hivi Mungu Baba akamwadhimisha mno kwa unyenyekevu wake. Basi mwaliko kwako ni amani na utulivu daima, na Mungu atakuadhimisha mno!

Katika Injili ya Marko katika historia ya mateso anatuwekea Yesu Kristu asiyejibu ubaya wowote unaoelekezwa kwake au kwa wengine kwa nguvu za kivita bali kwa neno la upendo. Tazama dhihaka ya Yuda Iskariote, tazama Mtume Petro anapotumia upanga kukata sikio la mtu aliye kinyume na Bwana. Yote haya anayajibu kwa utulivu na unyenyekevu wa hali ya juu akisema, rudisha panga alani!

Katika Injili ya Matayo tunamwona mwinjili akiweka mbele yetu msisitizo wa ukamilifu wa yale yaliyoaguliwa na manabii hapo kale juu ya Masiha, yakwamba atateswa na kisha kufa. Tunasoma hili katika aya ya 24: wakati wa karamu ya mwisho akishatangaza atakayemsaliti anamalizia akisema, “Naam, Mwana wa Mtu anakwenda zake kama maandiko matakatifu yasemavyo”.

Katika aya ya 56, pale Getsemane wanapomkamata, yeye mwenyewe anasema tena, “lakini haya yote yametendeka ili maandiko ya manabii yatimie, kisha wanafunzi wake wote wakamwacha na kukimbia”. Mwinjili Matayo anaweka mkazo katika hili kwa sababu anawaandikia Wayahudi akilenga kuweka vizuri dhana ya Masiha yakwamba tegemeo lao la Masiha mwenye utukufu na nguvu za kivita hayupo, bali mpole na mnyenyekevu wa moyo.

Anawajibu wale wote waliokwazwa na tendo la Masiha kuteswa, akileta hoja ya Agano la Kale ya kwamba ilikwishatangazwa na Manabii kwamba angetendewa hivyo. Mpendwa msikilizaji wewe uko upande gani? Upande wa Masiha mwenye siraha za kivita au mpole na mteswa? Tafakari!

Kwa kukaa katika upande wa Masiha mteswa basi unakubaliana na fundisho la Matayo akinukuu maneno ya Bwana, yaani rudisha panga alani. Jambo hili anaambiwa Mt. Petro, wakati huohuo Bwana mwenyewe anarudisha sikio la aliyekatwa. Masiha anamwambia Mt Petro asitumie upanga kamwe maana atumiaye upanga atakufa kwa upanga. (Mt. 26:52) Katika hili Bwana anatangaza amani na upole wa moyo mbele ya madhulumu. Kumbukeni mafundisho ya Origen katika karne za kwanza: “sisi wakristu hatuchukui mapanga tena, hatujifunzi tena kupigana vita kwa maana kwa njia ya Kristu Yesu tumekuwa watu wa amani”

Tunapata kusikia tu, katika Injili ya Matayo kifo cha Yuda Iskariote 27: 3-10). Yuda ni alama ya wafuasi wa Bwana ambao ni wa muda tu wakitarajia ushindi na mafanikio katika mipango yao na hivi Bwana anapoonesha kushindwa basi hukimbia na kumtafuta bwana mwingine ambaye kwa hakika ni kifo. Yuda anakata tamaa, haoni kwamba Bwana ni huruma upeo, kiasi kwamba angeweza kuomba msamaha kama yule mwizi wa msalabani.

Mpendwa msikilizaji, tukio jingine ambalo tunalikuta katika Injili ya Matayo tu, ni lile la kuwekwa walinzi katika kaburi la Bwana, Mt. 27:62-66) Hawa ni alama ya ushindi wa shetani. Yesu anaonekana kushindwa kabisa, na kupatilizwa katika kaburi. Hata hivyo Mungu ataingilia kati na kuonesha ushindi wa Mwanae wa pekee Mt. 28:4. Walinzi watashtushwa na mwanga mkali wa Pasaka na Bwana ataibuka kidedea akiwa mfufuka na mshindi wa vita dhidi ya shetani.

Mpendwa msikilizaji Mwinjili Matayo pamoja na Wainjili wengine wanatuwekea alama ya kupasuka kwa pazia la hekalu vipande viwili toka juu hadi chini akitaka kutuambia kuwa kwa njia ya kifo cha Bwana mipaka kati yetu na Mungu imeondolewa na si tu kati ya Mungu nasi bali kati yetu sisi kwa sisi. Tangu siku anakufa msalabani wote tu wana wa familia moja ya Mungu.

Mpendwa mwanatafakari ukiyakumbuka mateso ya Bwana na kuyaweka moyoni na kisha kuyaunganisha mateso yako na yake basi Pasaka kwako ni Ufufuko kweli. Ninakualika basi umsindikize Bwana katika Juma hili Kuu kwa furaha na utulivu mkamilifu ili mwisho wa mateso tupate matunda ndiyo uzima wa milele. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako toka Padre Richard Tiganya C.PP.S.

Siku za Vijana Duniani zinapania kukuza na kudumisha ari na moyo wa kimissionari

Baba Mtakatifu Francisko ana matumaini makubwa katika maadhimisho ya Siku za Vijana Duniani kama nyenzo msingi inayopania kuasha na kukuza ari na moyo wa kimissionari miongoni mwa vijana ndani ya Kanisa. Ni maneno ya Kardinali Stanislaw Rylko, Rais wa Baraza la Kipapa la Walei, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kimataifa wa wakurugenzi wa utume wa vijana, unaofanyika mjini Roma kuanzia tarehe 10 hadi tarehe 13 Aprili 2014. Mikutano hii ni sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani itakayoadhimishwa Jimbo kuu la Krakovia, Poland, kunako mwaka 2016.

Mkutano huu unahudhuriwa na wajumbe 250 kutoka katika Mabaraza ya Maaskofu Katoliki 90 na Jumuiya za Kitume 45 sanjari na Kamati ya Maandalizi ya Siku ya Vijana Duniani Rio de Janeiro na Kamati kutoka Jimbo kuu la Krakovia. Kardinali Rylko anasema, katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Kijimbo, itakayofanyika Jumapili ya Matawi, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Baba Mtakatifu Francisko atawakabidhi rasmi vijana kutoka Poland Msalaba wa Siku ya Vijana Duniani, uliotembezwa nchini Brazil kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko Brazil.

Tukio hili ni muhimu sana kwa mwaka huu, kwani Mama Kanisa anaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka thelathini, tangu Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, kunako Mwaka 1984 wakati wa Siku kuu ya Pasaka sanjari na kufunga rasmi Mwaka wa Ukombozi, alipowakabishi vijana Msalaba wa Mwaka wa Ukombozi. Ni Msalaba ambao umetembezwa sehemu mbali mbali za dunia kwa kuwasindikiza vijana katika shida na mahangaiko yao bila kusahau furaha na matumaini yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Msalaba wa Mwaka wa Ukombozi, umekuwa ni alama ya toba na wongofu wa ndani, chemchemi ya miito mitakatifu ndani ya Kanisa na kwamba ni Msalaba ambao kweli umekuwa ni kikolezo cha imani na matumaini miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, kama alivyosema Baba Mtakatifu Francisko nchini Brazil ni maadhimisho ya imani na udugu na kwamba, hii ni zawadi kubwa kwa Mama Kanisa.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 yatafanyika nchini Poland, miaka 25 tangu yalipofanyika kwa mara ya kwanza nchini Poland kunako mwaka 1991 mara tu baada ya kuanguka kwa Ukuta wa Berlin. Hapo dunia ikashuhudia nguvu na jeuri ya vijana waliomiminika kutoka sehemu mbali mbali za dunia ili kuungana katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, kwa pamoja wakaimba, ule wimbo maarufu "Abbà, Padre", unaoendelea kuvuma sehemu mbali mbali za dunia.

Tangu wakati huo anasema Kardinali Rylko, kumekuwepo na mabadiliko makubwa sana ulimwenguni na ndani ya Kanisa. Kuna mabadiliko makubwa katika ulimwengu wa vijana wanaoogelea katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Kumbe, maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ni kikolezo cha ari na mwamko wa kimissionari, kwa kutafuta na kuibua mbinu mkakati kwa ajili ya utume wa Mama Kanisa kwa vijana.

Kwa namna ya pekee, wakati huu, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kukazia umuhimu wa upendo na huruma ya Mungu; toba na wongofu wa ndani. Mama Kanisa anajiandaa kuadhimisha tukio la kihistoria kwa kuwatangaza Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuwa watakatifu hapo tarehe 27 Aprili 2014. Kanisa katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani itakayofanyika nchini Poland kunako mwaka 2016, itamkumbuka Papa Yohane Paulo II muasisi wa Siku za Vijana na Msimamizi wa maadhimisho ya Siku za Vijana Duniani.

Mwenyeheri Yohane Paulo II kwa vijana ataendelea kuwa ni Baba na Rafiki; Mlezi na Msimamizi wa vijana mbinguni. Mkutano huu umefanya pia tathmini ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani iliyofanyika Rio de Janeiro, Brazi, pamoja na kuangalia matunda ya shughuli za kichungaji yaliyopatikana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani nchini Brazil kwa njia ya ushuhuda na taarifa mbali mbali zilizowasilishwa na wajumbe.



Usilete mzaha, ananuka!

Manamuziki Remmy Ongala anakilalamikia kifo pasipo kutushauri tukikabilije: “kifo kifo kifo hakina huruma! Ukitaka kujua ubaya wa kifo, pita hospitalini, utakuta wengine wanalia. Wengine hawana miguu tena, wengine wana vidonda, wengine wana vipele, wengine wana ukurutu, wengine wamezaa watoto wamekufa shauri yako wewe kifo, kifo kwa nini unatusumbua. Tumezaliwa shauri ya kuishi. Ulimwengu bila watu siyo ulimwengu tena. Kifo we! Kifo kifo kifo hakina huruma…. Kifo ni kiboko yao!”

Ni ukweli kabisa, kifo hakina huruma, kifo kinatia uchungu, kifo kinakatisha tamaa ya maisha. Mbele ya kifo watu tunalia machozi. Ongala anakilaani kifo kiasi kwamba anaona hata magonjwa na ajali yanasababishwa na kifo. Ninakipongeza kifo kwa sababu kinatufanya watu wote tulingane! Kinamvaa kila mtu, bila kujali umri, cheo, ukuu, kabila, dini, jinsia. Kifo hakipokei rushwa. Ama kweli kifo ni kiboko kikali! Bahati mbaya na nzuri ya kifo kinawafanya wafiwa wengi wachanganyikiwe na kuanza kumlaani na kumtukana Mungu, kwa wafiwa wengine kinawakomaza kiimani na kimaadili. Hata kama tukilia na kulalalmika namna gani kifo kinabaki palepale na msimamo wake! Kifo ni suala nyeti. Je, haiwezekani kufanya appointment ya kukutana na kifo na kujadiliana naye suala hili nyeti?

Jumapili iliyopita tulitafakari “Ishara” jinsi anavyoita Mwinjili Yohana kuhusu uponyi wa upofu. Jinsi kipofu anavyozawadiwa mwanga au anavyofunguka macho. Ishara ile ilikuwa kama aina mpya ya uumbaji anaofanya Kristo. Lakini hata baada ya huko kufunguka macho, tunabakiwa bado na maswali dodoso ya kujihoji juu ya maisha. Mosi, Kristu anatufungua macho ili tuone nini au twende wapi? Pili, je, lengo la kutufungua macho ni kwa ajili ya kuona tu mambo hapa duniani halafu mwisho wake iwe nini?

Aidha, hata kama Yesu ananifungua macho na kuniwezesha kutembea vyema humu ulimwenguni, Je, maisha haya yana maana gani endapo hayana hatima? Je uzee usioisha na unaoendelea tu bila kwisha utauita ni ushindi dhidi ya kifo? Halafu hali hiyo ya uzee itaishia wapi wakati ulimwengu unaendelea kudumu tu hata bila ya mimi? Je, maisha hayo yanayoendelea tu yatakuwa na maana gani ndani yangu? Maswali kama haya ndiyo tutakayoyatafakari katika injili ya leo.

Tukitaka kuelewa vizuri hali halisi ya maisha tunayoyaishi, hatuna budi kuangalia kwa makini upi ni mwisho wake. Ni sawa na usafiri wa mguu usianze tu kusafiri kichwakichwa bila kujua wapi unaenda na umbali wake. Tunaposema mwisho wa maisha tunamaanisha kifo. Yaani, yabidi kukitafakari kifo, vinginevyo maisha yetu yote yanakuwa ni kutorokatoroka na kukikimbikimbia kifo, kwa kuogopa kukabili ukweli huo wa maisha ambao hatuna budi kuukabili.

Ni utamaduni wa binadamu ambao mara nyingi matendo ya maisha yetu yanajaribu kuepa kupanga ratiba ya kukutana na kifo. Kumbe, unaona kifo kinaendelea kututia wazimu hadi kutukosesha raha kabisa. Muziki wa Ongala unatupa hali halisi ya woga wa binadamu mbele ya kifo. Ni woga mkuu usioleta matumaini. Ama kweli “usilolijua litakusumbua.”

Ni ukweli dhahiri kwamba sisi binadamu tumeumbwa kwa ajili ya maisha ambayo hayana kikomo. Kwa hiyo ni vyema kukumbuka maneno ya mzaburi anayosema: “Ee Bwana utufundishe kuhesabu siku zetu, tujipatie hekima ya moyo” (Zab. 90:12). Tuwe na busara kutambua siyo kwa woga kwamba maisha yetu ni mafupi sana na tujaribu kuyapangilia vizuri.

Leo tumebahatika kuwa na mihadi (appointment) ya majadiliano na kifo kilichomwingia mwenzetu Lazaro. Msemaji mkuu katika mazungumzo hayo ni Yesu pamoja na wafiwa ambao ni dada wa damu wa mfu.

Tukifuatilia kwa makini mazungumzo hayo tutagundua uhondo uliomo katika ishara hiyo na kuelewa kifo ni nini na kina faida au hasara gani kwetu. Awali ya yote tuelewane juu ya matumizi ya msamiati wa neno kufufuka na tunavyolitumia kwa Lazaro. Hilo neno hapa siyo pahala pake kwa sababu neno kufufuka linamaanisha hali ya kupita toka ulimwengu huu na kuingia mbinguni kwenye maisha ya milele ya kukaa na Mungu Baba. Kwa mfano tunazungumza juu ya kufufuka kwa Yesu ikiwa na maana kwamba ameingia mbinguni na kuketi pamoja na Mungu Baba.

Kwa hiyo Yesu amefufuka yaani amepita toka ulimwengu huu na kuingia ulimwengu wa Baba. Kufika mbinguni na kumwona Mungu ni kikomo komesha na “Hakuna aliyemwona Mungu akarudi tena duniani.” Kwa hiyo kama Yesu alimfufua Lazaro ambaye alishaingia katika ulimwengu wa Baba basi alimkatishia mwenzake uhondo wa kukaa na Mungu. Kwa hiyo tunapozungumzia juu ya Lazaro, tusitumie neno kufufuliwa bali tutumie neno kuhuisha. Lazaro alihuishwa kwa sababu hakuwa ameingia katika maisha ya milele mbinguni.

Lazaro alirudishiwa uhai wake na akaendelea kuishi tena hapa duniani, ingawaje hatujui alikuwa wapi kipindi kile alichokufa na kuzikwa. Kati ya miujiza mingi aliyoyaifanya Yesu tendo hili la kuhuisha lilikuwa la pekee sana kwa watu waliolishuhudia, kwani watu walimwona Lazaro ameshafariki na kunuka. Mwinjili Yohani analichukua tendo hili la Yesu kuwa kama ishara, ili kuonesha jinsi gani Yesu ni Bwana wa maisha haya ya kibiolojia.

Hoja ya Yesu kumrudisha tena Lazaro katika ulimwengu huu wa maisha mapya ambayo hayakuwa yameguswa na aina ile ya maisha yenye malengo, yenye hatima, yaani maisha ambayo hayaishii hapa tu, bali yanaendelea na kuishia kwenye maisha ya Baba wa mbinguni. Huu ndio ujumbe mmojawapo ambao mwinjili anataka kutuletea katika ishara anayoifanya Yesu leo.

Sasa tuione kwa karibu ishara hii ya kuhuishwa kwa Lazaro. Masimulizi yanaanza hivi: “Kulikuwa na mtu aitwaye Lazaro.” Huyu Lazaro, alikuwa mwanafamilia ya namna yake. Kwa sababu katika familia hii hatuwaoni wazazi, yaani baba na mama. Tunaona tu kuna kaka na dada wawili Maria na Marta. Maana yake tunaoneshwa jumuia ya wana ndugu, au tungeweza kusema, jumuia ya kikristu. Jumuia ya kaka na dada ambao yabidi wakabiliane na hali halisi ya maisha. Hali halisi ya maisha tuionayo ni ya homa halafu kifo nk.

Katika familia hii tunasikia kuwa kaka mtu anaumwa homa kali inayopelekea kifo. Kabla mambo hayajawaharibikia, akina dada hawa wanatuma ujumbe kumtaarifu Yesu wakiwa na matumaini kuwa angemponya. Wakamwambia: “Bwana, yeye umpendaye hawezi.” Majibu ya Yesu hayaeleweki kirahisi, anaposema: “Ugonjwa huu si wa mauti, bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu.” Maana yake, kwa njia ya homa hii kutafumbuliwa kile ambacho Mungu anauwezo nacho na anachotaka kutufundisha. Kwa maneno haya Yesu anataka kusema kwamba yaonekana kuna ugonjwa unaopelekea kifo, na ugonjwa mwingine haupelekei kifo.

Ugonjwa unaopelekea kwenye kifo, ni ule unaoharibu maisha ya kweli ya mtu, yaani maisha yale yasiyo na mwisho. Kama vile isemavyo kwenye kitabu cha Mwanzo. Ukifanya uchaguzi wa mambo kinyume cha yale anayokuagiza Mungu utakufa: “Msile matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.” (Mwa 2:1) Kama hufanyi mambo kadiri alivyoagiza Mungu, unaharibu maisha yako halisi, maisha ya utu, ya binadamu. Huko ndiko kunakoitwa kufa-basi! Lakini kuna homa ambayo inakupeleka kwenye kifo cha kimwili tu (kibaolojia).

Kifo cha kimwili ni kile ambacho Mungu alishakipanga kwa ajili ya binadamu. Kifo cha aina hiyo hatuwezi kamwe kukikwepa. Hiki siyo kifo anachomaanisha Yesu. Ukweli Yesu aliipenda sana familia hii tena ni mapendo ya Kristu yanayotakiwa katika juimuia ya kikristu. Lakini unaona kuwa Yesu anaposikia kwamba Lazaro anaumwa, anabaki alipo na kuchelewa kwa siku mbili zaidi hadi Lazaro anakufa. Je upendo wa Mungu upo wapi pindi anatuacha tufe? Yesu anampenda Lazaro lakini anapomwacha afe anataka kutupa ujumbe. Hapa linaingia suala la ukuu wa Mungu.
Sisi tungependa kwamba Mungu aturuhusu tu tuingie paradisini pasipo kufa. Je, Mungu anaweza kuruhusu jambo hilo? Jibu ni hapana! Mungu angeweza kuruhusu hilo, lakini ingekuwa kama kutudanganya na kutuchanganya, kwamba Mungu anatupatia uhai huu ili aturudishie tena mwili huu wa kibinadamu tuendelee nao bila kwanza kuubadili kidogo. Tatizo ni kwamba, maisha yetu ya kibaolojia, yanahusu ulimwengu huu, lakini kwa vile ndani mwetu tuna maisha ya Kimungu, tunapopaswa kuingia katika maisha ya Mungu, kwa hiyo maisha haya budi yakome. Anayeshiriki maisha ya kimungu hawezi kufa, hawezi kupambana na kifo kile cha kibaolojia. Hadhi yetu ya kibidamu ipo kwa ajili ya kufa ili kuendelea na maisha ambayo Mungu ametuandalia.

Kwa kumwacha Lazaro afe, Yesu anataka kutuonesha waziwazi kwamba yeye hajafika kuzuia kifo hiki cha kibaolojia. Yesu anaacha mambo yafuate mfumo wake wa kimaumbile (wa kibaolojia). Mwanamuziki Mbaraka Mwinshehe anapowalilia wanamuziki waliofariki, anakubali kwamba kifo ni njia ya kila binadamu, anaimba: “Wanamiziki na wanamichezo wote hapa nchini Tanzania, hujiwa na majonzi kila mara tunapowakumbuka waliotutoka. Rambirambi zetu ziwafikie wanandugu. Kifo ni njia ya kila binadamu. Hatuna budi tutoe masikitiko na imani zetu kwa yao mazuri.” Kwa vile “Kifo ni njia ya kila binadamu”, Basi lengo la Yesu likatimia, kwani anapofika Bethania Lazaro alishafariki kitambo na kuzikwa siku nne zimeshapita.

Mandhali anayoikuta Yesu ni ya msiba. Hivi kulikuwa na watu wengi waliofika kuwatuliza wafiwa. Hapa unaalikwa kuvuta taswira (picha) kidogo ya hali halisi inayokuwa msibani, na ya watu wanaotuliza wafiwa. Mara nyingi watuliza wafiwa wanasema: “Poleni na msiba! Mtulizike ni mapenzi ya Mungu! Kazi ya Mungu haina makosa! Marehemu atabaki daima kwenye kumbukumbu ya mioyo yetu! Pengo lake haliwezi kuzibika tena! Sisi tulimpenda, lakini Mungu alimpenda zaidi! Bwana alitoa, na Bwana ametwaa, jina la Bwana na libarikiwe! nk.

Wakati mwingine inawekwa kanda ya muziki wa nyimbo za maombolezo. Pengine zinachapishwa hata kadi za ukumbusho na kuvaliwa sare za msiba nk. Yote hii ni kwa ajili ya kutuliza wafiwa. Lakini hata hivyo unaona wafiwa hawatuliziki sana wanazidi kuwa na majonzi na kubujika machozi. Hiyo ndiyo hali halisi inayoletwa na kifo. Kumbe ingefaa zaidi katika mazingira kama hayo kukitafakari kifo. Na katika misiba ya kikristu yatakiwa kutafakari kuhusu mwanga huu anaotupatia Kristu, yaani tumaini la ufufuko.

Hebu sasa tumfuatilie Yesu anapofika msibani anakabilianaje na mazingira haya magumu ya uchungu na huzuni? Atawatulizaje wafiwa hawa? Aidha wafiwa wenyewe wanamtazamaje Yesu aliyechelewa kufika licha ya kuambiwa hali ya mgonjwa kabla hajafa? Vituko anavyovionesha Marta kwa Yesu vinawakilisha vituko na fikra za wengi wanapokabiliwa na msiba au matatizo mazito. Mara nyingi tunasikia hata watu wa dini wanapokuwa katika matatizo, wanakosa imani, wanamkasirikia Mungu, wanakatishwa tamaa ya kuamini.

Angalia sasa Yesu anapofika pale msibani Marta anaanza kumvaa na kumgombeza bila hata ya kumwamkia: “Bwana kama ungalikuwapo hapa ndugu yangu hangalikufa.” Yesu anamwelewa vizuri tu Marta anajaribu kumtuliza kwa maneno aliyozoea kuyasikia mfiwa kadiri ya fikra za wengi ili aweze baadaye kuyatolea maelezo ya kina anamwambia: “Usijali ndugu yako atafufuka.” Kwa jibu hilo la Yesu, Marta anazidi kuchafuka nyongo tu, kwani haoni jipya kwa sababu alishakeremishwa ukweli huo kwenye imani ya mafarisayo juu ya ufufuko ujao kwa hiyo mara moja anamdakiza Yesu: “Najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho.” Ni dhahiri kwamba uelewa huu wa ufufuko ujao hauna maana yoyote.

Ufufuko utakaokuwepo sijui lini, yaani Mungu atuache tufe kisha baada ya kupita miaka mingi aturudishie tena maisha haya. Imani ya mtindo huu haiwezi kumtuliza mtu. Kutokana na udhaifu huo wa hoja ya ufufuko wa siku ya mwisho, Yesu anaongeza maneno yanayoleta maana na yanauyotuliza anamwambia kwa mkazo: “Mimi ndimi huo ufufuo na uzima.” Kumbe kama tuko gizani, basi tunahitaji mwanga toka nje unaoweza kutuangaza. Kujijulisha namna hii kwa Yesu kunafanana na kule alikomwambia yule Msamaritana pale kisimani: “Mimi ninayesema nawe, ndiye.”

Ni mimi niliye hapa ndiye ninayeweza kuhuisha mambo, ninayeweza kuwatuliza, wale waliokata tamaa ya maisha. Hapa mpangilio wa maneno unaanza na ufufuo halafu Uzima. “Mimi ndimi ufufuo na uzima”. Yaani kwanza kuwekwa huru halafu kuishi milele. Ufufuo ndiyo kitu cha muhimu zaidi katika maisha yetu ya sasa. Ufufuo ni mwito hasa kwa walio wazima kimwili halafu kwa waliokufa. Sisi tumeshakuwa wafufuka anavyosema Paulo: “Hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu, alituhuisha pamoja na Kristo; yaani, mmeokolewa kwa neema. Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu.” (Efeso 2:5-6). Ni kwamba mtu huyu amepata maisha au uzima ambao hauwezi kumtoka kutokana na kufa kibaolojia.

Maisha ya mbinguni ni bora zaidi kuliko maisha ya duniani. Jaribu kupata picha ya watoto pacha walio bado tumboni mwa mama. Humo tumboni watoto hao wanalishwa chakula toka mwilini mwa mama yao. Inapotokea kwamba mmoja anatangulia kuzaliwa, yule aliyebaki tumboni anaweza kuwaza kwamba mwenzangu amekufa. Lakini yule aliyezaliwa na kuona mwanga anaufurahia uso wa mama yake ambao kabla yake hakuujua ulivyo ingawaje mama yake huyo ndiye aliyekuwa anampa uhai alipokuwa bado tumboni. Sasa anauona laivu uso wa mama yake. Vivyo hivyo Yesu anaposema anayenisadiki mimi hatakufa anamaanisha kwamba baada ya maisha haya kuna maisha mengine utakayoyaona laivu.

Dada mwingine, Maria naye anafika kwa mtindo wake. Yeye anafika huku analia. Yesu anapomwona Maria analia anamwelewa kwamba hayo ni mapato ya kifo ndiyo yanayofanya mtu alie. Lakini kilio cha Maria na cha waombolezaje wengine ni kile cha sauti na cha kukata tamaa. Tofauti na kilio cha Yesu baada ya kuuliza: “Mmemweka wapi?” Yesu analia, lakini kilio chake hakikuwa cha kukata tamaa bali yasemwa yalikuwa yanamtoka tu machozi. Kwa hiyo hata mtu mwenye imani yatamtoka tu machozi mbele ya kifo. Baada ya kuelewana hivyo juu ya ufufuo na uzima, sasa Yesu anaanza kufanya vitu vyake ambavyo ndiyo ishara inayoonesha kuwa yeye ni ufufuo na uzima. Hapa Kifo kinakatwa kilimilimi.

Yesu anaagiza kuliondoa jiwe lililofunika pango alimowekwa mfu. Kuliweka jiwe juu ya pango maana yake ni kuliziba. Kitendo hiki cha kufunika kinatafsiriwa kuwa ni cha kusahau. Kwamba kesi ya mtu aliyekufa imeisha. Hebu ifunike! “Funika kikombe mwanaharamu apite”. Kumbe Yesu anaagiza: “Liondoeni jiwe.” Kwa sababu haina maana kuufunika kwa jiwe ulimwengu wa wazima katika shimo la “sahau” na kumtenga na ulimwengu wa watu walio paradizini. Martha anapata bado shida ya kuelewa maana ya kutoa jiwe lile wakati mambo yameishaharibika kabisa na yananuka.

Bado ana mashaka, akdhani kwamba mambo yataweza kumzidi Yesu. Anadadisi: “Ananuka kwa vile amekaa humo siku nne.” Marta hajui kwamba kunuka ndiyo pia ni hali halisi ya kifo. Yesu anamwambia: “Marta kama unasaidiki, utaona utukufu wa Mungu.” Baada ya kufunguka macho yabidi kuangalia mambo kwa undani zaidi na kuona mambo ambayo macho ya kawaida hayawezi kuyaona. Maana yake, kama unasadiki utaweza kuona.

Toka hapa sasa kunafuata mahitimisho ambayo ndiyo uhondo wa Injili yote ya leo. Yesu analia kwa sauti kuu: “Lazaro njoo huku nje.” Hiyo sauti ni kilio cha ushindi. “Mfu akatoka,” huyo anatamkwa jina la mfu na siyo kwa jina la Lazaro. Mfu alitoka aliyeviringishwa sanda miguuni, mikononi na uso umefungwa leso. Mfu huyo hatuoni wala sisi hatumwoni. Ameviringishwa nguo na kufunikwa leso kama vile mtoto mchanga aliyezaliwa.

Hapa ni dhahiri kwamba tunaletewa fundisho muhimu sana la kiteolojia, kwamba hata Lazaro amezaliwa toka tumbo la kaburi. Ni ukweli usiopingika kwamba Yesu amemhuisha Lazaro. Mwinjili anataka kurudia tena ishara ambayo Yesu ameitoa katika kitendo hiki cha kumfufua Yesu kuwa ni Bwana wa maisha, Bwana wa uzima siyo uzima huu wa kibaolojia wa kurudishia uhai Lazaro, la hasha, bali mwuujiza huo tuuchukulie kuwa ni ishara au kichokoo tu cha kutuonesha au kutushirikisha uzima mwingine ambao Yesu amekuja kutuletea hapa ulimwenguni. Mfu anakuwa mzima anazaliwa upya na anabaki katika hali ya mfu ameviringishwa vitambaa. Yaani mfu ambaye Yesu anamwita toka kaburini (pangoni) anabaki bado na alama zote za mzikwa wa kaburini. Kisha Yesu anasema: “Mfungueni, mkamwache aende zake.” Usemi huu nao ni muhimu sana. Tamko hili ni fumbo, kwani Yesu hasemi, “twendeni naye pamoja anakoenda huko”.

Baada ya tamko hili la Yesu na kumfungua mfu na kumwacha aende zake, tungetegemea kuona vituko vingine husika vikiendelea kuorodheshwa. Yaani tungemtegemea Yesu anaendelea kutoa maagizo yafuatayo: “Mfungueni halafu akisha jiweka sawa, ataweza kuja kutusimulia mambo yalivyokuwa kuzimuni alikokuweko siku hizi nne. Kisha tutaenda kumnywea na kufanya sherehe. Ratiba nyingine itaendelea jinsi mambo yatakavyojitokeza.”

Pengine hata Lazaro mwenyewe angeenda kumkumbatia Yesu ikiwa kama ishara ya shukrani. Lakini kumbe Yesu anasema tu “mfungueni na mkamwache aende zake.” Lazaro anaondoka na kwenda zake kimyakimya bila ya kuwahamasisha, au kuwachangamsha waliokuwa wanahuzunika.

Ndiyo mwisho! Ndivyo anavyotutendea Mungu, anayetuumba, anatuacha mahuru tuendelee na maisha bila kutufunga. Hii ni ishara kubwa katika maisha yetu ya kidini, kutomfunga Mungu katika imani, bali kumwacha huru. Ishara hiyo pia ni mwito kwa ndugu wanaolia na kuhuzunika kwa kuondokewa na ndugu, rafiki na mpenzi wao, lakini utakuwa ni ubinafsi mkubwa sana kumshikilia na kumtaka marehemu aendelee kubaki nao.

Yabidi kumwacha “kumfungua na kumwacha aende kwa raha zake.” Ingependeza sana kutanguzana naye kwenda pamoja huko aendako. Kumbe haiwezekani! Sisi tubaki tu kumsindikiza kwa jicho la imani katika hatua mbalimbali za maisha yake. Tumwache aende kwa uhuru wake wote. Ama kweli mwisho wa maisha ni mwanzo wa maisha.

Padre Alcuin Nyirenda, OSB



Kanisa linapania kushiriki kikamilifu katika kudumisha amani na majadiliano ya kidini huko Mashariki ya Kati!

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu jioni tarehe 7 Aprili 2014 amekutana na kuzungumza na Mfalme Abdullah wa Pili wa Yordan pamoja na ujumbe wake, ambao walipokelewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, aliyekuwa ameandamana na viongozi kadhaa kutoka Vatican.

Baba Mtakatifu na mgeni wake wamefanya mazungumzo yao kwenye Hostel ya Mtakatifu Martha, iliyoko mjini Vatican. Mazungumzo haya kadiri ya taarifa ya Padre Lombardi yamefanyika wakati viongozi hawa wawili wakiwa wanaendelea kupata chai ya jioni na kwamba, yamedumu kwa takribani dakika arobaini na tano.

Safari ya kikazi iliyofanywa na Mfalme Abdallah wa pili mjini Vatican ni sehemu ya maandalizi ya hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko huko katika Nchi Takatifu, ambako atapata fursa kwanza kabisa ya kutembelea na kuzungumza na wananchi wa Yordan na kwamba, wananchi wengi wa Yordan wanasubiri kwa hamu hija hii ya kichungaji, itakayomwezesha Baba Mtakatifu kujionea hali halisi ya wananchi wa Yordan.

Kwa upande wake, Baba Mtakatifu ameonesha utashi na nia ya kimaadili ya kutaka kushiriki kikamilifu katika mchakato unaopania kupata amani ya kudumu huko Mashariki ya kati pamoja na kudumisha majadiliano ya ya kidini, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Mwishoni, Baba Mtakatifu amesalimiana na wajumbe waliokuwa kwenye msafara wa Mfalme Abdallah wa pili wa Yordan



Unashangaa nini? Tazama!

Ninatumaini sisi sote tumewahi kuusikia msemo huu: “Funguka macho, Angalia!” Usemi huu hauna maana kwamba mmoja ni kipofu au amefumba macho yake na sasa anaambiwa ayafungue ili aweze kuona, la hasha bali ni “Kufungua Macho” ili kuweza kuona vyema mambo katika maisha. Mathalani, neno hili linaweza kutumika na wazazi wanaomwonya mtoto wao wa kike anayempenda mvulana mwenye matatizo labda ya kubugia unga, au wizi au hana maisha mazuri au mvivu na hataki kufanya kazi.

Mama mtu anaweza kumwangalisha bintiye na kumwambia: “Mwanangu, funguka macho. Je, huioni hali halisi ya maisha ya huyo kijana unayempenda? Angalia sana usije ukajitatiza. Utadhani umepata kumbe umepatikana!” Kwa hiyo, kuna upofu unaotibiwa hospitalini na mganga wa macho, lakini pia kuna upofu mkubwa unaokupotezea mwelekeo wa maisha, upofu unaokuzuia usiweze kuona hatari iliyo mbele unakoenda katika maisha, upofu ambao unakufanya usione na kuchukua uamuzi gani unaofaa wa kufuata. Maisha kwako yanakuwa giza. Unabaki kama kipofu unayeegemea ukuta, au mkongojo, au kuwategemea wazazi. Wakati kumbe mtu anayeona ni huru hamtegemei mtu yeyote yule.

Leo tutapambana na mganga mkuu wa tiba ya upofu wa macho wa aina hii ya pili. Tutapata mwongozo wa kujikwamua na upofu wa maisha kijumla. Mwinjili Yohane anatuletea kituko cha uponyi wa kipofu wa macho kwa namna kama ya tamthilia au mchezo wa kuigiza ili kutufafanulia vizuri maana ya upofu huo wa maisha na uponywaji unaofanywa na Yesu.

Yesu anajionesha kama mganga wa macho, mponyi wa upofu unaotuwezesha kuona vyema njia tunayosafiri katika maisha na kuchagua vyema maisha kadiri ya thamani zitakiwazo. Kuna usemi wa Yesu anaosema: “Pindi niko duniani, mimi ni mwanga wa ulimwengu. Yesu ni jua linalomeremeta na kutuangaza sote.” Kutokana na ukweli huo, Injili ya Yohane inafungua kwa neno hilo la mwanga: “Kulikuja nuru amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu. Yohane mbatizaji hakuwa nuru, bali alikuja kuishuhudia tu ile nuru yenyewe.” (Yoh 1:7-9).

Kristo ni mwanga unaotuwezesha kuona vyema maisha kwa namna inayoipa maana ya maisha yetu. Injili hii daima ilikuwa inatumika jumapili ya leo katika safari ya wakatekumeni watakaobatizwa Jumamosi Kuu. Baada ya kuibuka toka kwenye kisima cha ubatizo wakawa wanaitwa walioangazwa, wanaomeremeta. Yaani wale waliokuwa wamepata zawadi ya mwanga toka kwa Kristu! Waliofunguliwa macho juu ya kuuona vizuri ulimwengu.

Yawezekana kabla yake walikuwa wevi, wadanganyifu, wachakachuaji, wala rushwa, lakini bila kujitambua kuwa ni vipofu wakapotea njia, wakawa wanapuyanga porini tu hata hawajui wanakoelekea. Sasa wanafuata Injili ya Kristo inayowafungua macho yao. Hali ambayo tunaweza kuipata hata sisi, tunapokosea, kufanya uchaguzi usiofaa katika maisha, anafika mmoja na kutufungua macho, anapotuambia “Angalia, Kaa chonjo, Jihadhari,” hapo tunashtuka kwani tungekosea halafu mapato yake yangekuwa mabaya. Huo ndiyo ufunguo wa kuelewa fasuli ya Injili ya leo.

“Yesu alipokuwa anapita alimwona kipofu tangu kuzaliwa.” Hatuambiwi jina la mtu huyo, bali anatajwa tu kuwa ni kipofu, anaweza kuwa mtu yeyote yule. Maana yake hiyo ni hali ya kibinadamu, ya mtu yule ambaye hajakutana na Yesu, amezaliwa kipofu. Mtu wa namna hiyo, hawezi hata kuhitaji mwanga au nuru, kwa sababu haufahamu ulivyo kwa sababu hajauona. Wakati mwingine tunaweza kusikia watu wakisema: Mume wangu haendi kabisa Kanisani kusali, na hana hata wazo la kusoma biblia au kusikiliza mazungumzo ya mambo ya dini. Au unakutana na mtu, anakuambia “mimi sina hamu kabisa na ukristo, yaani sina interest kabisa!”

Hilo si jambo la kushangaza, kwa sababu Mtu ambaye hajauona mwanga, (kipofu) hajakutana na Kristu, itakuwa ni kumdai mno mtu wa namna hiyo (kipofu) atamani kuutazama ulimwengu kwa namna tofauti. Kwa sababu hana wazo, hawezi kufikiri namna nyingine, hawezi kujua, ni kitu gani hiyo nuru. Mtu aina hiyo ni kipofu anahitaji kufunguka macho. Ni sawa na mtu anayekuja kugundua uhondo wa muziki, uhondo wa riadha, uhondo wa kufanya hija, uhondo wa kusoma hesabu, uhondo wa siasa, nk. Kabla yake hakuwa anashabikia chochote, sasa utamkuta anafurahia kwa sababu kuna mtu amemfungua macho – anakuwa limbukeni hana siri.”

Wanafunzi wa Yesu wanapomwona huyo kipofu wanakuwa kama waafrika mbele ya matatizo, wanaanza kumtafuta mchawi, wanamwuliza Yesu: “Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake hata azaliwe kipofu?” Hebu angalia kwa makini jibu la Yesu ni tofauti kabisa na fikra zetu. Anajibu kifupi tu: Hiyo ni hali halisi ya maisha. Kwamba mtu anazaliwa hivyo. “Hiyo ni kazi ya Mungu.” Mwanga huu unatoka mbinguni, siyo jambo analoweza kulileta binadamu. Yawezekana akaendelea kuwa kipofu hivyo hadi kufa, au kuweza kubahatika kukutana na Kristu anayeweza kukufungua macho kwa neno lake.

Yesu hataki kusikia watu wanazungumza juu ya dhambi kama inavyozoeleka kusikia kwamba, dhambi imeingia duniani kwa njia ya wazazi wetu wa kwanza na hivi sisi sote tuko katika dhambi, la hasha, bali sisi tunazaliwa hivyo. Yesu anatualika kufunguka macho, kuangalia nuru ya Mungu daima, na ni yeye pekee anayeweza kutufungua macho na kuona ulimwengu kwa namna ya pekee.“Baada ya kusema hayo, Yesu alitema mate chini na kufanya tope kwa yale mate. Kisha akampaka kipofu kope za macho”. Tendo hilo ni muhimu sana, kwa vile inarudiwa kusemwa mara tano katika fasuli ya Injili ya leo Yesu alitema mate chini na kufanya tope kwa yale mate.

Tumeshasikia mara nyingi katika Agano la kale, juu ya tope, ya pumzi ya Mungu na mate. Hayo yanamaanisha uhai au uzima. Kitendo kilichofanyika cha Mungu alipomwumba Adamu. Yesu anakirudia kitendo hicho ikiwa kama ni uumbaji upya wa mtu mpya. Sasa mtu mpya anazaliwa kutokana na mwanga wa Kristu. Yaani sasa mtu anaishi kama inavyotakiwa kuwa binadamu. Anajua anakotakiwa kwenda kisha anamtuma huyo kipofu na kumwambia: “Nenda kanawe katika birika ya Siloamu, maana yake aliyetumwa.” Wataalamu wanasema Siloamu maana yake siyo aliyetumwa, neno kutumwa lingekuwa shaluak ambacho ni kisima pekee kilichokuwa katika mji ule wa Yerusalemu.

Hapa kwa neno hilo mwinjili anataka kuonesha maji yale ambayo yanamfungua macho, kama maji ya ubatizo, na yule ambaye anampa mwongozo wa kuyapata hayo maji yaani Roho wa Kristu, yaani maisha ya kimungu ambayo yanakuwezesha kuona hali halisi ya maisha. Baada ya kutoka kisimani kunafuata mfululizo wa vituko vinavyomsibu kipofu huyu aliyepona. Hiyo ni sawa na safari ya mtu anayeona mwanga baada ya kufunguliwa macho na Yesu. Mtu anayesafiri peke yake bila kutegemezwa na Yesu. Safari ya kipofu huyu ni sawasawa na safari yetu wakristu kuelekea mwanga. Unaalikwa kutanguzana kipofu huyu ujifunze kutembea vyema baada ya kupata mwanga wa ubatizo ili kuelekea kwenye mwanga halisi wa maisha.

Kulikuwa makundi kadhaa ya watu waliokuwa wanahoji na kuujadili uponyi wa kipofu huyu kwa namna yao. Kikundi cha kwanza alichopambana nacho huyu kipofu ambaye sasa anaona ni cha majirani waliokuwa karibu sana naye: Watu hao wanaonekana sasa kutokuwa na uhakika kama wanayemwona ndiye aliyekuwa kipofu mwombayala maskini au la, wanaulizana: “Je! Huyu siye yule aliyekuwa akiketi na kuomba? Wengine wakasema ndiye. Wengine wakasema, La! lakini amefanana naye.”

Tunaweza kujiuliza, je, kumetokea nini hadi Mtu huyu hatambulikani tena na jirani zake alioishi nao. Hiyo ndiyo historia ya maisha yetu, hiyo ni hali halisi ya maisha yetu. Historia ya wale waliokuwa vipofu ambao walikuwa wanatembea bila kuelewa wachukua uchaguzi gani mzuri wa maisha. Wanapofunguka macho katika nuru ya Kristu, wanakuwa watu tofauti kabisa hadi kutokutambulikana tena na watu aliozoeana nao kabla.

Yawezekana mtu alikuwa anathamini mambo mengine kabisa ya duniani, magari, nyumba, raharaha, lakini sasa amegundua thamani nyingine bora zaidi za maisha. Labda alikuwa mpiga rushwa, au mchakachuaji, mdanganyifu, sasa ni kinyume chake. Sasa amefunguka macho. Hivi unapokutana na wanaomfahamu, wanaweza kubishana wenyewe kwa wenyewe. Ni yule au siyo yule tunayemfahamu? Maana yake mtu aliyeangazwa kweli, anakuwa tofauti kabisa kwa sababu yuko katika safari kuelekea mwanga.

Wanapomwuliza Kipofu huyo anathibitisha kwamba ndiye: “Mimi ndiye”. Watu hao wanataka kujua “Kulikoni” wanamwuliza “Yalifumbukaje”. Naye anarudia kueleza ilivyokuwa: Mtu yule aitwaye Yesu alifanya tope akanipaka macho akaniambia, Nenda Siloamu ukanawe; basi nikaenda na kunawa, nikapata kuona”. Inakuwa vizuri sasa hata mimi ninapoulizwa swali la mtindo kama huo imekuwaje hadi uwe mkristu, ulipatapataje wito wa ukristo, wa utawa, wa ukatekista au upadre?

Kipofu anaendelea na safari yake ya maisha. Mara anakutana na kikundi cha pili cha watu ambao ni viongozi wa kanisa. Yaani watunzao mapokeo yadini na ambao tungetegemea wangestaajabia kumwona aliyekuwa kipofu sasa anaona. Kumbe hao wanachukizwa na mtu aliyemfungua macho kipofu huyu. Kikundi hicho cha pili siyo cha wengine bali ni cha Mafarisayo: Chuki yao inakuja pale wanapotambua kwamba, huyu kipofu kabla yake alikuwa anafuata amri zao, alikuwa anafanya wanachotaka wao, alikuwa amewategemea kumbe sasa amefunguka macho, anaona mambo kwa namna tofauti.

Hao ni maadui wa nuru, wanawawakilisha wale walio wafungwa wa fikra zao, dhana zao, mawazo yao juu ya Mungu. Wamefungwa katika utamaduni na mapokeo yao na hawataki kubadili kitu. Hapo wanasema mtu aliyemponya kipofu siyo mtu wa Mungu kwani hashiki sheria ya sabato ya mapokeo yetu. Hivi wanamhoji: “Mafarisayo nao wakamwuliza tena jinsi gani alivyopata kuona.” Naye kipofu anatoa majibu yaleyale aliyotoa mwanzoni: “Alinitia tope juu ya macho nami nikanawa, na sasa naona.” Wanapobishana wao kwa wao juu ya mtu huyo wanagawanyika na wanashindwa kupata jibu wanalolitaka, wanamwuliza tena kipofu mara ya pili, “Wewe wasemaje katika habari zake kwa vile alivyokufumbua macho?” Kipofu anatoa jibu linalompa cheo zaidi Yesu: “Mimi kwa binafsi yangu naona kuwa mtu huyu: ‘ni nabii’”.

Kikundi cha tatu ni wazazi wanaoitwa na wafarisayo na kuulizwa maswali: Wazazi wanamfahamu vizuri sana mtoto wao. Viongozi wanawauliza wazazi “Huyu ndiye mwana wenu, ambaye mnasema kwamba alizaliwa kipofu? Amepataje, basi kuona?” Wazazi wanaruka swali la pili na kulijibu la kwanza: “Tunajua ya kuwa huyu ndiye mwana wetu, tena ya kuwa alizaliwa kipofu; lakini jinsi aonavyo sasa hatujui. Wala hatujui ni nani aliyemfumbua macho. Sisi hatumo katika suala la kufunguka kwake macho. - Mwulizeni yeye mwenyewe, yeye ni mtu mzima, atajisemea mwenyewe.” Yaani alizaliwa kipofu, na kuna mwingine amemfungua macho”.

Hapa unaona kama vile wazazi hawa wanaogopa, wana woga wa kuponywa. Wanamwogopa kijana anayeona mambo kwa namna ya pekee kuliko namna ile waliyomfundisha wao. Wazazi wana wasiwasi, kwa sababu wale ambao hawafuati mapokeo wanaweza kufukuzwa toka hekaluni. Hapa unaweza kuwakumbuka watu ambao wametoa mchango mkubwa sana katika jamii, katika siasa lakini hawapokewi vizuri. Mwanga ni hatari, unagombanisha watu.

Kinakuja kikundi kingine cha nne ambacho ni kilekile tena cha mafarisayo, wanamwambia yule kipofu: “Mpe utukufu Mungu.” Ni sawa na kusema: “Umshukuru Mungu”. Maana yake, wewe kiri tu kwamba umekosea, kisha sisi tutajitahidi kuweka mambo sawa. Hasahasa kurekebisha kufuru hii iliyojitokeza kwa sababu “Sisi tunajua ya kuwa mtu huyo ni mwenye dhambi.”

Hapo kipofu anaanza kuitetea hali halisi anayojisikia kuwa nayo, yaani hali ya kuona mwanga mpya wa Kristu aliyemfungua macho hayo. Anawapa ukweli wao: “Kwamba yeye ni mwenye dhambi hilo mimi silijui. Najua neno moja, kuwa mimi nalikuwa kipofu na sasa naona.” Hapo tunajifunza kwamba yabidi kwa haki yote kujiacha kutetewa na matendo na siyo kwa sheria. Unaona wazi kuwa mtu huyu aliyepata mwanga sasa anazidi kuwa na uhakika zaidi wa mambo na kujiamini zaidi.

Wanapomwulizia tena jinsi alivyofumbuka macho wanapomwuliza: “Alikutendea nini? Alikufumbua macho jinsi gani?” Wanataka aendelee kujibu, ili waweze kutafuta mwanya wa kumkosoa. Hapo yule kipofu anawashtukia na kuwapa “makavu laivu”. “Nimekwisha kuwaambia, wala hamkusikia; mbona mnataka kusikia tena? Yawezekana labda na ninyi mnataka kuwa wanafunzi wake?” Ni kitu cha kawaida kutoa majibu haya makavu. Na kutoka hatua hii sasa wanaanza kutupiana lugha za kebehi na matusi ya rejareja. “Wewe ndiye mwanafunzi wake, sisi tu wanafunzi wa Musa. Sisi tunajua ya kuwa Mungu alisema na Musa; bali yule hatujui anakotoka.” Mafarisayo daima wanakimbilia kusema: “Sisi tunajua” na huyu kipofu daima anasema “Mimi sijui”. Watu wanaofikiri kwamba daima wanajua yote hawawezi kupata mwanga, watabaki daima kuwa katika giza.

Wafarisayo wanaposema kwamba hawajui anakotoka Yesu, kipofu anawakebehi tena na kuwaambia: “Hii ni ajabu! Ninyi mnaojua mambo yote, lakini hamumjui anakotoka huyu aliyenifumbua macho!” Ni kama anawaambia: “Tunakichojua sisi wenyeji yaani watu wa kawaida ni hiki kwamba, mcha Mungu (anayemwogopa Mungu) daima anasikilizwa na naye Mungu.

Aidha, haijawai kusikika kwamba kumetokea mtu anayafumbua macho ya mtu aliyezaliwa na hali ya kipofu. Asiyetoka kwa Mungu hawezi kutenda neno lolote.” Kutoka kwenye hali ya kebehi hadi wanafikia kukashifiana na kutoleana lugha chafu. Hawa wafarisayo, wanashindwa kuhimili vishindo wanaamua kumfukuzia nje. Ni namna dhahiri ya kutenda ya mtu asiyetaka kufunguka macho na kuuona mwanga. Ukifuatilia mazungumzo haya utaona jinsi yalivyopanuka kidogokidogo kutoka kwenye ushawishi, kebehi na dharau matusi hadi kuchefuana nyongo na mwisho kumfukuza mtu. Ndiyo mtindo wa kufanya mambo mtu asiyetaka kufunguka macho. Kipofu anaondoka, anajiona kuwa huru anatoka nje.

Katika sehemu ya mwisho ya Injili tunasikia kwamba yule kipofu akakutana tena na Yesu. Lakini ukweli ni kwamba Yesu alimtafuta yule kipofu ndipo walipokutana nje walikofukuziwa wote wawili. Yesu anaenda kumtafuta mwenzake ambaye naye amefukuzwa kama yeye. Anajua kuwa yule anayepokea mwanga, hawezi kutazamwa vyema na watu wa mapokeo. Yesu akamwuliza: “Wewe wamwamini Mwana wa Mungu?” Yaani wewe unajiaminisha kweli kwa mtu aliyekufungua macho? Yule kipofu anajibu “Ni nani, Bwana, nipate kumwamini?”. Yesu anamjibu: “Umemwona, unayesema naye ndiye.” Mtu aliyeangazwa hahitaji tena uwepo wa mwalimu. Alikuwa ameongozwa katika safari yake na ile Injili inayoendelea kumfungua macho. Ndugu yangu, katika safari yako ya maisha funguka macho uongozwe na nuru ya Kristo yaani Neno lake.
Alcuin Nyirenda, OSB.


Tafakari ya neno la Mungu, Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima

Niko nawe tena katika kipindi tafakari masomo Dominika ya IV ya Kipindi cha Kwaresima, ambapo tunaalikwa kuwa watu wa mwanga. Katika somo la kwanza tunakutana na uteuzi wa kiongozi atakayeongoza taifa la Israeli.

Mpendwa mwana wa Mungu, jambo hili linatokea miaka 1000 kabla ya Kristu wakati ambao Waisraeli walikuwa katika shida na taabu. Ili kuweza kuondokana na taabu hizi walilazimika kutafuta kiongozi atakayewasaidia kuwaongoza ili waweze kupata ushindi toka Wafilistini. Kwa njia ya Samueli Mungu anaonesha kijana mmoja toka Betlehem katika ukoo wa Yese, ambaye atapakwa mafuta kwa ajili ya kuwa mfalme wao.

Basi Nabii atakwenda mpaka Betlehem na kumwambia habari hii Yese ya kwamba mmojawapo wa wanawe amechaguliwa na Mungu kuongoza taifa la Israeli. Yese anapokea habari hii kwa furaha kuu. Katika furaha hiyo, Yese anafikiri na kuona kwa mtizamo wake, kuwa mtoto huyu atakuwa ELIABU. Katika hali ya kawaida, Eliabu alikuwa mrefu na mzuri, tena alikuwa mtoto wa kwanza. Samweli anavutiwa na sura ya Eliabu, lakini Mungu anasema hapana!

Kwa hapana ya Mungu, Yese atalazimika kuwaleta watoto wake wote isipokuwa Daudi aliyekuwa machungani! Mpendwa msikilizaji, kati ya watoto hawa walioletwa hakukuwa na aliyechaguliwa na Mungu na hivi Samueli akamwambia akamlete Daudi. Yese kwa kuamuliwa amlete Daudi alisema bado Daudi ni mdogo kwa utume ambao ni mkubwa namna hii! Lakini Nabii atasisitiza kuwa huyu ndiye chaguo la Mungu.

Mpendwa, katika uchaguzi huu tunagundua kuwa njia za Mungu na njia zetu ni tofauti kabisa. Fikiria kwa kuchagua taifa la Israeli liwe taifa teule aliacha taifa imara kiuchumi yaani Babilonia, akaacha Misri lililokuwa taifa lenye ufundi wa hali juu na lenye watu wa dini, (Deut, 7:7-8). Ni katika mlengo ule ule katika AJ Bwana atawachagua maskini, wadhambi, wanaoteswa, na wanaotengwa kwa ajili ya ufalme wake. Kumbuka pia alipozaliwa watu wa kwanza kushuhudia utukufu wake ni wachungaji waliokuwa kondeni. Mpendwa msikilizaji, ndiyo kusema hatuna mamlaka ya kuingilia mpango wa Mungu, ni vema siku zote tukajisalimisha katika yeye kadiri ya mapenzi yake.

Katika somo la Pili Mtakatifu Paulo anawaandikia Waefeso akisema, kwa njia ya ubatizo wametwaliwa toka giza na kuingizwa katika mwanga. Kwa tendo la kuingizwa katika utawala wa mwanga, wanaalikwa kuishi na kutenda matendo ya mwanga na kuachana na matendo ya aibu. Anasonga mbele akisema lazima kukemea matendo yaliyo ya aibu tena katika uwazi na kuyapatilizia mbali.

Katika Injili tunakutana na picha ya kipofu anayeponywa na Bwana. Jambo la msingi na fundisho la Bwana ni kwamba yeye amekuja kuwaondolea watu upofu wao na hasa upofu wa kiroho. Tunaona kabla ya tendo hilo jema, wafuasi wake watamwuliza wakisema: Bwana, hivi ni nani kati ya mtoto kipofu na wazazi wake aliyetenda dhambi mpaka mtoto yuko hivi?

Wanauliza swali hili kwa sababu kulikuwa na imani kwamba Mungu huwaadhibu wenye dhambi na kuwarehemu wema! Ndiyo kusema magonjwa na mikosi ilikuwa ni tokeo la dhambi! Aidha, aliyezalwa katika shida kama hizo alidhihirisha kuwa dhambi ilitendwa na wazazi pamoja na mababu. Mpendwa mwana wa Mungu, kufikiri hivi ni kinyume cha mapendo ya Mungu kwa watu, kwa hakika Mungu hajui kuadhibu bali kupenda tu. Ndiyo kusema shida zilizopo zinakuja kwa sababu ya uzembe wetu na hivi lazima tutafute suluhisho na namna ya kukabiliana nazo.

Katika sehemu ya pili ya Injili tunaona sasa ukamilifu wa kile alichokifundisha, yaani anakiweka katika matendo. Katia kutenda mwujiza wa kumfanya kipofu aone tena, anatema mate chini na kufanya tope ambalo atampaka kipofu. Baada ya hilo anamwambia nenda kanawe katika birika ya Siloamu na kwa kufanya hivyo kipofu anaona! Mpendwa msikilizaji, kuna nini katika matendo haya? Mambo yako hivi kwa sababu watu wa wakati huo waliamini katika pumzi kuwako na roho na katika mate kulijaa nguvu ya mtu.

Ndiyo kusema Bwana anatumia alama zilezile kutenda kazi yake ya kuleta uhuru kwa kipofu. Bwana haishii tu katika alama hizi za mwanzo bali anamwambia nenda ukanawe katika Siloamu, ndiyo kusema anamtuma. Hapa tunaona Bwana aliyetumwa na Mungu anamwalika mtu kuja kwake ili apate maji ya uzima, maji yanayoponyesha kama alivyomwahidia mwanamke msamaria, na kisha kwenda kutangaza habari njema ya furaha.

Baada ya tendo hili la uponyaji kipofu ataulizwa na watu mbalimbali kuhakikisha ni kwa nguvu ya nani amepona. Wa kwanza ni majirani zake ambao wanajiuliza ni yeye au ni mwingine na baadaye watampeleka kwa Mafarisayo ambao watamlalamikia Bwana badala ya kumsifu, ati kwa sababu alitenda kazi hiyo wakati wa Sabato, na kwa jinsi hiyo Bwana hakutoka kwa Mungu. Katika hili wengine walisema lakini inawezekanaje mwenye dhambi afanye mwujiza huu?

Kwa majirani kipofu atasema mimi ndiye na wala si mwingine. Kwa Mafarisayo atasema yakuwa aliyeniponya ni Nabii. Mpendwa msikilizaji, katika kuendelea kutafuta ukweli, wenye madaraka watawaendea wazazi wake na kuwauliza na wazazi kwa woga wa kutengwa watasema kamwulizeni yeye mwenyewe kwa kuwa ni mtu mzima. Wenye mamlaka watamrudia aliyekuwa kipofu wakitaka akane ukweli na yeye atawaambia ninachojua ni kwamba nilikuwa kipofu na sasa ninaona. Ndugu huyu aliendelea kutetea ukweli huo kwa furaha mpaka mwisho.

Mpendwa, katika hili twajifunza kuwa wakweli na kuwa wenye furaha daima, na hivi kusimamia imani na matendo makuu ya Mungu. Ndiyo kusema furaha na neema za Mungu tulizozipokea kwa njia ya ubatizo na kipaimara twapaswa kuzitunza mpaka mwisho wa nyakati. Tena, katika safari ya kulinda imani kutakuwa na wakati wa furaha na mateso, jambo kuu ni kuweka tumaini katika yeye aliyetuponya.

Mpendwa ninakutakia furaha na matumaini katika maisha yako daima ukimtanguliza Mungu na kwa nguvu zake kukua na kusimamia imani uliyoipokea kama zawadi toka kwake.

Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.


BAADA YA KUSOTA, BATAROKOTA AULA TUZO ZA KILL MUSIC AWARD


HATIMAYE mwanamuziki  Batarokota amefanikiwa kuingia kwenye tuzo za muziki za Kilimanjaro Music Award mwaka 2014, kwa mujibu wa waandaaji wa tuzo hizo, Batarokota ameingia na wimbo wake Kwejaga nyangisha.

Tayari makundi ya washiriki wa tuzo hizo yameshapangwa hukua akichuana na wanamuziki wengine wenye majina makubwa hapa nchini, makundi hayo yanahusisha wanamuziki maarufu kama Diamond lakini kundi la Batarokota lipo kama ifuatavyo.

Wimbo bora wenye vionjo vya asili ya Kitanzania
1 Kwejaga nyangisha-Batarokota
2 Nalonji-Kumpeneka
3 Bora Mchawi-Dar Bongo massive
4 Tumbo lamsokota-Ashimba
5 Aliponji -Wanakijiji
6 Agwemwana-Cocodo African music band

Batarokota amekuwa katika mafanikio mazuri baada ya kutengenezxa wimbo huo kupitia njia ya video, hivi karibuni alifanya ziara yake ya kimuziki katika nchi za Swaziland na Afrika Kusini.

Diamond awacharukia tuzo Kili


Kutajwa kwa msanii Diamond Platnumz kuwania tuzo sita za Kilimanjaro 2014, hakujatosha kumfunga mdomo msanii huyo asizungumzie kutofurahishwa kwake na maamuzi ya kutoswa katika tuzo hizo kwa nyimbo za wasanii Snura, Madee na Jux.

Nyimbo za wasanii hao 'Nimevurugwa', 'Tema Mate Tuwachape' na 'Uzuri Wako', zimepigwa marufuku kuonekana katika televisheni na kuondolewa katika kinyang'anyiro cha tuzo hizo na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kutokana na video zake "kukosa maadili" ya Mtanzania.

Kupitia kurasa za mitandao yake ya kijamii, Diamond ambaye ameingia katika tuzo hizo kupitia wimbo wake wa 'My Number One', aliandika: "Ikiwa kweli tuna lengo la kutoipotosha kimaadili jamii yetu na vizazi vyetu pendwa, nafikiri ni vyema tungeanza kuzuia video na nyimbo za kutoka nje, kuliko kuzuia nyimbo na video za nyumbani ambazo uchafu wake haufikii hata robo ya uliopo kwenye nyimbo zinazopewa kipaumbele kutoka nje... Hii ni sawa na kuzidi kuukuza muziki wa nje huku tukiudidimiza na kuua muziki wetu... Mikakati ya kufikia malengo yetu itafanikiwa kweli?? #Ni_mtazamo_tu"

Mwanamke Msamaria anakutana na "Kyasaka"



Mwanamuziki Mbaraka Mwinshehe, aliimba: “Ugeni tabu ndugu zangu, unapofika nchi za mbali huwa mashaka. Hapo fikira za nyumbani hukujaa tele na majonzi kukujia mengi. Ugeni tabu mi’ nasema kweli si masihala wasafiri waelewa. Kwani unaweza tafuta kazi ukapata na pakulala ukawa huna. Ukabaki kuhangaika usiku kucha kwa sababu ya ugeni. Kweli nyumbani ni nyumbani nchi za kigeni hazina mazoea.” Wimbo huu unaonesha ukweli anaopambana nao msafiri au unapojikuta katika mazingira mazingira mageni ambayo wenyeji wake wanakushangaa na hawako tayari kukupokea.

Mtu ukiwa mgeni katika mazingira au pahala usipozaliwa yaani katika mazingira ya taifa jingine au hata kabila jingine, unaweza ukaitwa majina mengi sana hata majina ya kebehi, unawezwa ukaitwa mtu wa kuja; kyasaka, mnyamlenge, mpoma, mgeni, nk. Kama ni mgeni katika mazingira ya dini nyingine, hapo unaweza kuitwa kafiri, mromani, likristu, nk. Kwa vyovyote kuwa mgeni ni karaha sana hasa kama hutaki kujipokea na kujikubali kwamba wewe ni mgeni, mnyamlenge, mtu wa kuja, mpoma, kafiri, mkristu, mromani, nk. Unahitaji pia busara au diplomasia ya hali juu sana ili kuweza kuyatawala mazingira hayo, na hatimaye ukaweza kuyaathiri mazingira ambayo kwa mwanzoni yalikuona kwa jicho baya au hayakukupokea.

Leo tutakutana na mwanadiplomasia na mwanasaikolojia mkuu aliyepambana na mazingira mazito sana ya ugeni, lakini akafaulu kuyateka na kuyabadili. Injili inamwonesha Yesu kama mnyamlenge katika nchi ya Samaria. Alikuwa ametoka kusini Judea (Uyahudini) anaelekea nyumbani kwake kaskazini Galilea, hivi kwa vyovyote ilimbidi akatishe kana kupita katikati ya nchi ya Samaria. Hapo ndipo kilipompata kisanga cha kujisikia mgeni kwenye ardhi hiyo. Siyo tu yeye alijisikia mgeni bali alionwa hivi kama mtu wa kuja, mtu wa utamaduni tofauti na wasamaria tena na mwanamke. Watu wa makabila hayo mawili Wasamaria na kabila la Yesu (Wagalilaya) walikuwa hawaivani kabisa kiutamaduni. Zaidi tena Yesu alitazamwa kama mtu mwenye imani au dini tofauti na ile ya wasamaria yaani walitofautiana kiitikadi.

Katika mazingira kama hayo, utaona jinsi Yesu alivyo gwiji wa saikolojia anavyoweza kukabiliana na mazingira magumu, anavyosikiliza, anavyohoji mambo, na kutoa rai zake, hadi anafikia hali ya kuanzisha mazungumzo (dayalogu) mazuri yanayolainisha na kugeuza moyo mwa mpinzani wake. Hali ambayo ni kama kuanzisha “uzao upya”. Mnaweza kirahisi kulinganisha na kutofautisha dayalogu au mazungumzo yalivyokuwa kati ya Ibilisi na Yesu kule jangwani (Dominika ya kwanza kwaresima) na mazungumzo haya ya kati ya mwanamke huyu msamaria na Yesu kwenye kisima (chemchemi) ya maji.

Mapato ya mazungumzo ya hapa kisimani, yanatokana na uhuru aliokuwa nao Yesu, hadi kufanikisha kuathiri mazingira yaliyokuwa magumu sana tena yaliyokuwa dhidi yake. Hali hii inaonesha wazi kwamba Yesu ni mwalimu wa utu kwa wote, mdiplomasia na msaikolojia mkuu. Ni mwalimu kwa sababu anao uweza wa kuvuka vizuizi vinavyopinga majadiliano. Mipaka au vizuizi vile vinavyomtenga mwanaume na mwanamke, mipaka kati ya watu wa eneo moja hadi jingine; kati ya watu wa makabila tofauti. Ukitaka kujifunza utu wema, saikolojia na diplomasia ya kweli na kuweza kuanzisha na kuendesha dayalogu ya aina yoyote hata ile ya kisiasa, basi jaribu kufuatana na Yesu katika Injili ya leo.

Mchokozi rasmi wa majadiliano hayo ni Yesu anayeomba: “Nipe maji ninywe”. Majibu ya mwanamke yule ndiyo yanayoonesha kuwa Yesu ni mtu wa kuja katika kabila jingine: “Imekuwaje wewe mgeni kuniomba mimi maji ya kunywa, nami ni mwanamke Msamaria?” Jibu kama hili linatosha kabisa kukukatisha tamaa na kuendelea kuomba maji. Mwanamke huyu anamwonesha Yesu kuwa hawana mahusiano yoyote kikabila wala kijinsia. Kwani kati ya myahudi rabi na mwanamke haikuwezekana wala haikuruhusiwa kabisa kuzungumzana. Kumbe Yesu akiwa kama mwalimu wa uzima kwa sababu Yeye ni chemchemu unapotoka uzima. Anaanzisha mazungumzo na kukutanisha watu ambao wamekata kabisa mawasiliano, wala kupeana mikono. Yesu anaanzisha mazungumzo na mahusiano kwa kuanza na ufukara wake: “Nina kiu” (Nipe maji ninywe). Tujifunze kutoa kama anavyotoa Yesu. Kama mtu fukara anayepokea, kutoa kwa fukara, kwa watu wa kuja (wageni) na siyo kwa ukuu kama ule wa mtu tajiri, bali kwa unyenyekevu wa watu fukara. Anayejua kuwa anaweza kupokea zaidi endapo anajali utu. Yesu anafaulu kumzaa mwanamke mpya. Anapozungumza na wanawake anawagusa moyo moja kwa moja. Anajua lugha zao, lugha ya kutamani lugha ya vionjo, lugha ya kutafuta hoja nzito za kuishi.

Kuhusu kupambana na ugeni wa mazingira ya imani (dini) tofauti, ni pale Yesu anapokubaliana na kauli ya mwanamke kwamba anaishi na mshikaji wa sita baada ya kuachika na washikaji wengine watano “Hapo umesema kweli.” Hapo mwanamke anaanza kuthibitisha kutofautiana kwao katika imani: “Baba zetu waliabudu katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia.” Tamko hili la mwanamke linaonesha wazi kwamba wao ndiyo wanaofuata mapokea ya mababu ya kuabudu katika mlima, wakati dini ya Yesu ni maagizo ya watu wa siku hizi waliojijengea tu hekalu Yerusalemu na kuabudu. Yesu anachukua mwanya huu wa kutofautiana kiitikadi za imani na kumfundisha mwanamke yule akisema: “Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi. Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli...” Hapa Yesu anaenda zaidi ya pale anapofahamu mwanamke na kumwongezea uhondo zaidi wa kuabudu, yaani kuabudu Baba katika roho na kweli.
Ndipo sasa unapomwona Yesu anaibuka na namna mpya ya saikolojia, anaweza hata kupendekeza jambo linalohusu maisha binafsi ya mtu anapomwambia mwanamke: “Nenda kamwite mumeo, uje naye hapa.” Hapa ndipo mwanamke akajibu “Sina mume” kwa kweli angetakiwa aseme tu kwamba “Ninaye mshikaji.” Mwanamke huyu ni mithili ya wayahudi waliokuwa wametangaanawakilisha wale wanaoabudu miungu, sanamu, ni sawa na malaya. Mwanamke huyu ni mimi!

Yesu anasema: “Umesema vema, ‘Sina mume’; kwa maana umekuwa na waume watano naye uliye naye sasa siye mume wako; hapo umesema kweli.” Yesu hamhukumu yule mama msamaria tena hamdhalilishi, bali anasisitiza karibu mara mbili kwa kusema “Umesema kweli kabisa”. Yesu alishamtambua mwanamke huyo ni wa aina gani kutoka mwanzo alipofika kuketi pale kisimani mchana. Wanawake wa kawaida wanachota maji asubuhi sana au jioni, kwa hiyo anayeenda kuchota maji mchana tena peke yake anaweza kujulikana ni mwanamke wa aina gani na anatafuta nini. Kwa tamko hilo “Umesema kweli kabisa” Yesu hana nia ya kuharibu mahusiano waliyo nayo, bali anataka kumweka sawa mwanamke huyo kwamba hana budi kujiweka sawa kabla ya kujidhatiti kuyawania hayo maji ya uzima anayoyatamani. Aidha siyo Yesu anayetakiwa kuyapanga maisha ya mbele ya huyo mwanamke – bali ni kama vile angemwambia “Kazi kwako!” Upendo ni mlango wa Mungu na ni Mungu aliye ndani yetu. Ni Mungu anayetujali sana, ni Mungu mwenye utu wa hali ya juu sana, hiyo ndiyo sura nzuri ya Mungu.

Mwanamke alisema kuwa “Kisima kile ni kirefu kimezama sana.” Kiasi Yesu asingeweza kufanikiwa kuchota maji kwa vile hakuwa na kata (nyenzo) ya kuchotea. Endapo kisima hicho ni wewe na mimi, hapa unaona dhahiri kwamba ipo njia moja tu ya kuchota maji ya kisima hicho kilichozama sana cha kila mmoja wetu, nayo siyo kwa njia ya kugombeza, kukashifu, kukosoa, bali kwa njia ya kumfanya mmoja aonje utamu zaidi wa maisha, wa uzuri wa mali au kisima alicho nacho. Angalia Yesu anavyomtamanisha mwanamke huyu hadi anachoka mwenyewe anapomwambia: “Mimi nitakupa maji ambayo yanakuwa chemchemu”. Maji ni uzima, maisha, nguvu ya maisha, ambayo ninaipokea ninapojiunganisha na chemchemi isiyokauka ya maisha ambayo ni Mungu. Yesu anampa Mama Msamaria fursa ya kujiunganisha au kujisogezasogeza karibu na chemchemi yake ili baadaye yeye mwenyewe awe chemchemu.

Hiyo ni picha nzuri sana, picha ya maji yanayotembea, inayobubujika, mto wa uzima ni zaidi ya ule unaozima kiu yako tu, bali ni mto ule unaozima hata kiu ya wengine. Chemchemu haimilikiwi bali inajieneza, inazaa. Kwa ahadi kama hiyo ya Yesu, yule mwanamke msamaria anaelewa kwamba hataweza kutuliza kiu yake kwa kunywa na kusaza, bali kwa kutuliza kiu ya wengine. Kwamba ataangazwa tu kwa kuangaza wengine, atapata furaha kwa kutoa furaha kwa wengine. Kuwa chemchemi: ni mradi mzuri wa maisha, ni chemchemi ya matumaini, ya kupokea, ya upendo. Baada ya kuuelewa ukweli huu juu ya chemchemi, hapo ndipo sasa, mwanamke yule anautelekeza mtungi wa maji pale kama vile ungekuwa kitenge kilichochakaa, anaacha maisha ya zamani, anakimbia kwenda mjini na kumsimamisha kila anayepita barabarani. “Jamani! kuna mtu kisimani huko, anayekuwezesha uzaliwe na kuzaliwa tena upya. Usipozaliwa hujaumbika. Njoni mumtazame mtu aliyeniambia mambo yote niliyoyatenda.” Anakuambia mambo yaliyoko katika moyo wako na kuiibusha chemchemi.

Mwanamke huyu anahaha huku na huku, anakimbiakimbia, anaita, anashuhudia, anafanya unabii, anawachemsha watu wote, na hadi anazungukwa na jumuia mpya ya kwanza ya wafuasi wageni. “Basi wakatoka mjini, wakamwendea.” (Yohane 4:30). Na katika mji ule Wasamaria wengi walimwamini kwa sababu ya maneno ya yule mwanamke aliyeshuhudia kwamba, “aliniambia mambo yote niliyoyatenda.” Basi wale Wasamaria walipomwendea, walimsihi akae kwao; Watu wengi zaidi wakaamini…” (Yoh 4:39-40). Kuna mmoja, Yesu, anayejua na kusema yote juu yako. Yeye anajua kilicho ndani ya mioyo yetu: Jema lina nguvu zaidi kuliko bovu au baya, kuna jema lililo kongwe zaidi kuliko ubaya, kuna jema linawezekana kuwa muhimu zaidi kuliko ubaya wa sasa. Kuna ziwa la nuru na uwepo wake ndani mwetu ndiyo unaokuwa chemchemu.

Kwa hiyo nitaenda wapi ili kuwambudu Mungu? Siyo mlimani, siyo hekaluni au Kanisani!. Bali katika mimi: ni mimi ndiye ule mlima wa Mungu, mimi ni Kanisa. Naye ni chemchemi ya chemchemi zangu. Hata sisi, kama yule mama msamaria, anayeenda kisimani kuchota maji na anarudi ametajirika, kama tukimpokea Mungu ndani yetu anayetufanye tuzaliwe upya, anayebomoa kila kizuizi, mpaka, hapo tutaona kububujika kati ya mikono yetu wimbo wa chemchemu. Pahala popote pageni utakapokuwa, hali yoyote ile chukivu, mtazamo wowote ule mbaya wa maisha utaweza kuubadili kwa mazungumzo ya upendo, bora tu ukijifunza toka kwa Yesu.
Padre Alcuin Nyirenda, OSB.

Siku kuu ya toba, wongofu na upatanisho!


Kama ilivyokuwa kwa Manabii, wito wa Yesu wa toba na wongofu wa ndani haulengi kwanza kazi za nje yaani kuvaa gunia na kujipaka majivu, kufunga na kujitesa, bali wongofu wa moyo unaogusa undani wa mtu mzima. Bila wongofu huu, matendo ya toba hayana nguvu wala ukweli ndani yake. Wongofu wa ndani husukumwa kuonesha ishara zinazoonekana, vitendo vya mwili, na kazi za toba.

Toba ya ndani ni kuelekeza upya kabisa maisha yote, ni kurudi na kumwongokea Mwenyezi Mungu kwa moyo wote, kukataa dhambi na nafasi zake; kuchukua maovu, kwa kujiwekea lengo ka kubadili maisha pamoja na kuendelea kutumainia huruma na neema ya Mungu. Wongofu wa ndani hufumbata maumivu na machungu ya wokovu ambayo Mababa wa Kanisa wameita kuwa ni taabu ya roho au toba ya moyo.

Moyo wa mtu ni mzito na mgumu. Inatakiwa Mwenyezi Mungu ampe mtu moyo mpya. Ikumbukwe kwamba, wongofu wa ndani ni kazi ya neema ya Mungu inayoufanya moyo wa mwanadamu uweze kumrudia tena Muumba wake, kwa kugundua ukuu, huruma na mapendo ya Mungu yasiyokuwa na kifani. Mwamini anapaswa kuonesha masikitiko ya dhambi zake, kwa kumwangalia Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kwa Damu yake azizi, Yesu amemkomboa mwanadamu na kuukirimia ulimwengu neema ya toba na wongofu wa ndani.

Mama Kanisa amewawekea watoto wake nyakati za toba zinazojikita katika mazoezi ya maisha ya kiroho, liturujia, hija, kujinyima, kufunga na kusali pamoja na kushiriki katika kazi za matendo ya huruma na kimissionari. Kwa kutambua umuhimu wat oba na wongofu wa ndani, Baba Mtakatifu Francisko, ametenga Ijumaa ya tarehe 28 Machi 2014 kuwa ni siku maalum ya toba na wongofu wa ndani, mwaliko wa kuchuchumilia Sakramenti ya Upatanisho, inayomwonjesha mwamini huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani.

Hii ni mikakati ya shughuli za kichungaji inayotekelezwa na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji Mpya. Baba Mtakatifu Ijumaa, majira ya jioni ataongoza Ibada ya Upatanisho kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na baadaye atapata fursa ya kuungamisha baadhi ya waamini watakaoshiriki katika Ibada hii na baadaye kutoa ondoleo la dhambi.

Kuanzia majira ya Saa mbili kamili asubuhi, Kanisa la Mtakatifu Agnes, Bikira Maria, Trastevere na Kanisa la Madonda Matakatifu, yataendelea kutumika kwa ajili ya Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kwa muda wa Masaa 24. Hayo yamesemwa na Askofu mkuu Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji Mpya. Ni tukio ambalo litawahusisha vijana ambao kimsingi ni Wainjilishaji wapya kwa kuwakaribisha vijana wenzao, kuingia ndani ya Kanisa, ili kuonja huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Ndani ya Makanisa haya, watakutana na Mapadre ambao watakuwa tayari kuzungumza nao na hatimaye, kuwaungamisha.

Tukio hili la kihistoria, anasema, Askofu mkuu Fisichella, litahitimishwa kwa Ibada ya Masifu ya kwanza ya Jioni, Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima, Ibada itakayofanyika kwenye Kanisa la Santo Spirito in Sassia, Jimbo kuu la Roma.