MAANDALIZI ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania mwaka huu ni ya kipekee
kutokana na kupambwa na mbwembwe nyingi ikiwamo misafara na maandamano
makubwa ya wagombea urais. Ni jambo la kujivunia kuona kwamba wananchi
wengi wameonyesha mwamko mkubwa wa ushabiki wa kisiasa.
Hadi sasa dalili za awali zinaonyesha kwamba ushindani mkubwa wa
kinyang’anyiro cha urais utakuwa kati ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na
Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Misafara na maandamano makubwa ya wagombea urais hao vinazidi kuteka
akili za wananchi wengi waliogawanyika katika makundi mawili
yanayoelekea kulingana; kundi linalomshabikia Lowassa na jingine
linalomuunga mkono Dk. Magufuli.
Kutokana na misukumo mikubwa ya hisia za kisiasa, kuna wananchi ambao
ukiwambia kuwa Dk. Magufuli ndiye rais ajaye wanaweza kukutoa roho!
Vivyo hivyo, wapo wengine ambao wakikusikia unasema njia ya Lowassa
kuelekea Ikulu ni nyeupe wanaweza kukutenga katika jamii.
Ukiuliza sababu za wanaoamini kwamba Lowassa atashinda urais
watakwambia ni misafara na maandamano makubwa ya watu wanaoonekana
kumshabikia. Hata kwa upande wa Dk. Magufuli jibu ni hilo hilo!
Lakini kwa upande mwingine, wapambe wa Lowassa wanamuelezea kwamba ni
mwajibikaji na mwenye uamuzi mgumu katika masuala ya umma, hivyo anafaa
kukabidhiwa uongozi wa nchi kwa ajili ya kuboresha maisha ya Watanzania
kiuchumi na kijamii.
Wengine wanaamini kwamba Dk. Magufuli ndiye anafaa kukabidhiwa mikoba
ya Ikulu ya Tanzania baada ya Rais Jakaya Kikwete. Kwamba mgombea huyo
ni msafi asiye na kashfa za ufisadi, lakini pia hayumbishwi katika
kusimamia misingi ya uwajibikaji kwa umma na kutetea maslahi ya Taifa.
Kimsingi hakuna wa kuwalaumu mashabiki wa pande hizo mbili maana
wanatekeleza haki yao ya kikatiba na kidemokrasia ilmradi hawavunji
sheria za nchi.
Lakini pamoja na haki hiyo, mashabiki hawa wanapaswa kutafakari vizuri
juu ya misimamo yao ya kuamini kwamba misafara ya kifahari na maandamano
makubwa ya watu ni kielelezo tosha cha ushindi kwa mgombea urais.
Si sahihi kutumia takwimu za idadi kubwa ya watu katika misafara na
maandamano kuwa ndiyo kigezo cha ushindi kwa mgombea, maana mbwembwe za
aina hiyo hazimchagui rais. Kinachomchagua rais ni kura zinazopigwa kwa
utaratibu uliowekwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), si vinginevyo.
Tukumbuke kwamba mtu yeyote ana uhuru wa kushiriki maandamano ya
wagombea urais, ubunge na udiwani bila kuulizwa kitambulisho. Lakini
haruhusiwi kupiga kura za kuchagua viongozi wa nafasi hizo kama hana
kitambulisho husika na iwapo atakiuka maelekezo ya NEC.
Hii ni sawa na kusema kwamba katika Tanzania hii, kila mtu, yaani
mwenye kitambulisho cha kupiga kura, asiye nacho, mtoto na hata mgonjwa
wa akili, wote wana uhuru wa kushiriki maandamano ya wagombea, jambo
ambalo ni tofauti na utaratibu wa kupiga kura za kuchagua viongozi wa
kisiasa.
Ikumbukwe hata wakati wa ziara ya Rais Barack Obama wa Marekani hapa
Tanzania Julai 2013 maelfu ya watu walijitokeza kumlaki, kumwona na
kusikia anachosema, ingawa si kweli kwamba wote walikuwa wanampenda wala
kumkubali na kumfurahia. Miongoni mwao walikuwapo wanafiki
waliochukizwa na ziara hiyo wakiamini kimakosa kwamba alikuja kusaini
mikataba ya kuuziwa nchi yetu!
Misafara na maandamano ya wagombea ni sawa na kokoro ambalo wakati
mwingine hubeba viumbe wasiohitajika. Kuna watu wanashiriki misafara na
maandamano ya aina hiyo wakiwa na dhmira ya kweli ya kuwaunga mkono
wagombea, lakini wengine wanakwenda kufanya kazi zisizo za kisiasa kama
vile kulinda usalama, kupiga picha, kurekodi video na sauti.
Kwa hiyo, kuamini au kujitumainisha kwamba idadi kubwa ya watu kwenye
misafara na maandamano ya wagombea ndiyo kigezo cha ushindi, ni sawa na
ndoto za mchana kweupe ambazo daima hazitimii.
Itakuwa jambo la maana kama mashabiki na wapambe wa kisiasa
watazingatia umuhimu wa kujitokeza kwa wingi kupiga kuza za kuwachagua
wagombea wanaowataka kuliko kujiridhisha na wingi wa watu katika
maandamano ambayo hayana nafasi ya kuchagua viongozi.
Kuamini kwamba idadi kubwa ya watu kwenye misafara na maandamano ya
wagombea ndiyo kigezo cha ushindi ni dhana potofu na matokeo yake mwisho
wa siku upande unaoshindwa katika uchaguzi hudhani umeibiwa kura, na
wakati mwingine hugeuka kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani usiyo wa
lazima.
Jambo la msingi zaidi kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu ni
kuongeza juhudi za kuhamasishana (kwa wenye vitambulisho
waliojiandikisha kwenye dafrari la kudumu la wapigakura) kujitokeza kwa
wingi kupiga kura za kuchagua viongozi tunaowataka siku ya Jumapili
Oktoba 25, mwaka huu.
Sambamba na hilo, wananchi wote tunapaswa kushiriki mikutano ya kampeni
za wagombea kutoka vyama mbalimbali vya siasa ili kuwachuja na kubaini
wanaofaa kutuongoza baada kusikia sera na ilani za vyama vyao.
Ingawa baadhi ya wananchi imani zao zimejikita kwenye vyama, lakini ni
vizuri zaidi kuchagua mtu kwanza, chama baadaye kwa sababu maendeleo na
mabadiliko tunayoyataka yataletwa na viongozi watu, siyo vyama ambavyo
daima haviwezi kufanya chochote.
Lakini pia, tushirikiane kuuombea Uchaguzi Mkuu ujao baraka za Mungu
ili ufanyike kwa uhuru na haki. Tuombe tukitambua kwamba mshindi wa
uchaguzi huo atakuwa ni yule aliyepigiwa kura nyingi kwa utaratibu
halali, si vinginevyo. Mungu ubariki Uchaguzi Mkuu Tanzania 2015.