
Mkurugenzi wa Takukuru, Edward Hoseah.
Rushwa sio suala la kupeana fedha chini ya meza, kwa msingi usio wa
halali, na kwa mtu asiyestahili; kupeana huduma kwa upendeleo au kwa
kutaka kulipwa kitu fulani kwanza; au hutoa huduma kwa misingi ya udugu,
familia, mapenzi, ukabila, dini. Lakini rushwa ni matokeo, sio chanzo
cha matatizo.
Kama rushwa ni mtoto wa chanzo fulani, basi madhara yanayotokana na
rushwa ni mjukuu wa chanzo ambazo TAKUKURU wanatakiwa kukimaizi na
kukishughulikia. Lakini kama mnaweza!
Niliwahi kuandika kuwa, Rushwa ni mtazamo- a frame! Mtazamo huu
umejenga fikra za kiitikadi na kujikita katika fikra za wananchi kiasi
kwamba, hatuoni namna ingine ya kuishi ila hiyo ya kutoa rushwa.
Na TAKUKURU wanapokuja na mtazamo kinzani- challenger frame, kuwa
rushwa ni jinai, ni makosa, wanakuta sisi tuko tayari tumeshajikita
katika utamaduni wa kutoa rushwa.
Ni sehemu ya maisha, ni mazoea- practice. Na kwa kweli hatuoni kuwa
binadamu anaweza kuishi bila kutoa au kupewa rushwa. Na mazoea haya
yana msingi wa kihistoria katika uchumi na siasa.
Kuna wakati nchi hii, ilikuwa na uchumi mzuri sana. Wakati ule
tulisema dola moja ilikuwa sawa na shilingi tano; dala! Noti ya shilingi
ishirini ilikuwa ikiitwa pauni; pauni moja ilikuwa sawa na shilingi
ishirini.
Nchi hii ilikuwa bora katika uzalishaji wa bidhaa za walaji kutoka
viwandani na mashambani. Nchi ilikuwa na viwanda na ajira kwa sisi
tuliokuwa tunamaliza masomo haikuwa shida. Nchi ilikuwa na wanasiasa
ambao kazi yao ilikuwa ni kufikiria namna gani viwanda, kilimo na huduma
vitoe ajira kwa wananchi.
Nakumbuka wakati ambao nikiwa likizo ya masomo niliweza kupata kazi
ya muda viwandani. Nakumbuka tulipokuwa tunamaliza masomo yetu tulikuwa
tukijaza fomu za kuomba kupelekwa kwenye ajira mbalimbali- CEL Form.
Ikaja kufa. Viwanda vilikufa, kilimo kilikufa na sekta ya huduma
ikafifia. Nchi ikaharibu uchumi wa viwanda vyake kwa kuruhusu soko
lifanye kazi yake. Wanasiasa waliona kuwa kazi ya kufikiri juu ya uchumi
sio yao tena bali ya IMF, WB na nchi wahisani.
Sisi sio wa kufikiri tena bali kufikiriwa. Wanasiasa hawakukaa na
hawakai kutafuta majibu ya matatizo yetu, bali kuandika bajeti ambayo
wafadhili watajiridhisha kuwa tunafaa kukopeshwa au kupewa msaada;
kufanya maandiko ya miradi kwa ajili ya ufadhili.
Fedha ikawa inaingia serikalini. Wanasiasa badala ya kufikiria
kuziongeza kwa kufanya uwekezaji wa kiserikali- public sector
investment, wakaona sasa aliye mjanja na mwenye meno awahi hizo fedha.
Wakakimbilia kununua hisa kwenye viwanda, mashirika, na kununua
mapande ya ardhi na kuyalimbikiza. Fedha zilizoingia serikali hazikuwa
tena kwa ajili ya kuzizungusha kama mtaji bali kugawana kwa wale
wanaojua zilipo na namna ya kuzichota.
Na ajira ikawa sasa kwa undugu, urafiki, mapenzi, ukabila. Ndio tunasikia hayo ya watoto wa vigogo BOT.
Wanasiasa wakaona siasa ndio sekta pekee ya kuiwekea fedha za
kutosha- lakini sekta za afya, elimu uzalishaji wa kilimo na viwanda na
huduma, hakuna. Nchi ikaanza kushindwa kusafirisha bidhaa nje; tukaanza
kuwa waagizaji; ajira na uzalishaji vikapungua, tukaambiwa tuwe
wajasirimali kwa ajili ya soko ambalo limejaa bidhaa za nje tayari.
Aidha viongozi wamekuwa sasa ndio wanaolindana sasa. Wote ni wale
wale. Kama hakuna utashi wa kisiasa wa kupigana na rushwa kwa maana ya
(i) kutooneana aibu, (2) kutafuta majibu ya kuuokoa uchumi unaodorara,
(3) kusaidia taasisi za kupambana na rushwa- polisi, Usalama wa Taifa na
TAKUKURU, kufanya kazi kwa meno halisi badala ya kutumia ya bandia,
mnawezaje kuiondoa rushwa.
Sitaki kuwa mtu mwenye kejeli- cynical, kuhusiana na hili. Huu ndio
ukweli niuonao, na niuonavyo. Hatuwezi kupambana na rushwa, nasubiri
siku rais aseme sasa imetosha na rushwa ni adui wa haki.
Na atakayesema, uchumi na ukue, atakayesema sasa imetosha. Hayupo
na hatapatikana kama wale wanaotoa rushwa ndio wanaoweza kupitishwa kuwa
rais Oktoba 2015.